Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Aaga Mwili wa Mbunge Irene
Apr 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 27 Aprili 2022 ameshiriki Ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maaalum Mkoa wa Rukwa, Marehemu Irene Ndyamkama aliyefariki dunia tarehe 24 Aprili 2022. Ibada ya kuaga mwili wa mbunge huyo imefanyika katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.

Akitoa salamu za rambirambi za serikali, Makamu wa Rais ameipa pole familia ya Irene Ndyamkama, Spika wa Bunge, Naibu Spika, Wabunge pamoja na waombolezaji wote kufuatia kifo cha mbunge huyo na kuwaomba kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Aidha, Makamu wa Rais amesema Wabunge wanapaswa kujifunza yale mema aliyoyafanya marehemu Irene Ndyamkama wakati wa uhai wake ikiwemo kuwajali wale wanaoishi katika mazingira magumu kama vile yatima na wajane.

Makamu wa Rais amesema kila kiongozi anapaswa kujifunza maisha ya uzalendo kwa taifa kwa kutumikia vema nafasi anayopata kama alivyofanya Irene Ndyamkama enzi za uhai wake. Pia ametoa salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi ambao wameguswa na msiba huo.

Kwa Upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema marehemu Irene Ndyamkama alikua mfuatiliaji wa kazi zake kwa mawaziri ili kuwasaidia wale anaowawakilisha Bungeni. Waziri Mkuu amewaasa  Wabunge kumuombea ili apumzike kwa amani pamoja na kumuenzi kwa kuendeleza yale mema alioyafanya katika utumishi wa Bunge kipindi cha uhai wake.

Awali, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Tulia Ackson amesema Marehemu Irene Ndyamkana aliishi maisha ya ukamilifu kwa kuishi vema na watu. Ameongeza kwamba mbunge huyo alijaaliwa utu, upendo na heshima hali inayofanya kumkumbuka wakati wote na kushukuru kwa maisha yake hapa duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi