Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majimbo 214 Kunufaika na Ugawaji wa Vifaa Tiba vya Shilingi Bilioni 14.9
Jan 05, 2024
Majimbo 214 Kunufaika na Ugawaji wa Vifaa Tiba vya Shilingi Bilioni 14.9
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (anayehojiwa) akizungumza leo Januari 5, 2023 wakati wa kuzindua usambazaji wa Vifaa Tiba (nje ya vilivyopangwa kununuliwa kwenye Bajeti ya 2023/2024) vitakavyosambazwa katika majimbo yote 214 nchini Tanzania Bara.
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu leo Januari 5, 2023 amezindua usambazaji wa Vifaa Tiba (nje ya vilivyopangwa kununuliwa kwenye Bajeti ya 2023/2024) vitakavyosambazwa katika majimbo yote 214 nchini Tanzania Bara.

Amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha za nyongeza shilingi biilioni 14.9 mwezi Novemba 2023 na kununuliwa vifaa hivyo ili kuendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

“Tunategemea kupokea vifaa tiba vingine hivi karibuni ambavyo ni vitanda vya kujifungulia (4280), vitanda vya kufanyia uchunguzi (examination table) 4280, mkoba wa vifaa vya kujifungulia (delivery kit) 4280, kabati za vitanda (bed side lockers) 6420 na stendi ya dripu (6420)” amebainisha Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema takwimu zinaonesha asilimia 86 ya wanawake wajawazito Tanzania wanajifungulia katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri, vifaa hivyo vitakwenda kusaidia kuboresha huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.

Ameongeza, kila jimbo litapata vitanda 30, magodoro 30, mashuka 60, bed side locker 30, drip Stand 30, meza ya kulia chakula 15, vitanda vya kujifungulia 10, delivery set 10 pamoja na examination bed 10.

“Waheshimiwa Wabunge watavikuta vifaa hivi kwenye vituo viwili katika kila jimbo ambapo Bohari ya Dawa (MSD) watashusha mzigo huu”, amesema Waziri Ummy.

Vilevile, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Sekta ya Afya kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya ambapo imeweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

“Vifo vimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000 ikiwa lengo la dunia ni Tanzania kupunguza vifo vya wajawazito kufikia vifo 70 kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.

Miongoni mwa vifaa ambavyo Waziri Ummy amepokea ni pamoja na vitanda vya wagonjwa 3,080, vitanda vya kujifungulia 1,000, magodoro 5,500, mashuka 36,808, pamoja na meza za vutanda 306.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi