Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maafisa Ustawi wa Jamii Fanyeni Kazi kwa Weledi- Dkt. Biteko
Sep 06, 2023
Maafisa Ustawi wa Jamii Fanyeni Kazi kwa Weledi- Dkt. Biteko
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Serikali na wa Sekta binafsi.
Na Mwandishi wetu - Dodoma

Maafisa ustawi wa jamii nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo mbalimbali ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii ili kuwezesha utoaji wa huduma bora.

Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Serikali na wa Sekta binafsi uliolenga kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto za kada hiyo na kuleta ustawi wa wananchi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi zinazotoa huduma za Ustawi wa Jamii nchini uliofanyika jijini Dodoma tarehe 6 Septemba 2023.

“Wapokeeni wahanga wa matendo ya ukatili, migogoro ya ndoa na mirathi na wahitaji wote wa huduma za ustawi wa jamii kwa upendo na kuwasikiliza vizuri ili kubaini kiini cha matatizo wanayopitia na kuwasaidia. Kutokana na changamoto wanazopitia baadhi yao wanakuwa wameanza kuathirika na tatizo la afya ya akili hivyo ni jukumu lenu kuwahudumia kwa upendo na kuwaonesha utu’’, amesisitiza Dkt. Biteko

Ameongeza “Natoa rai kwa watu wote na taasisi zinazotoa huduma za ustawi wa jamii katika vituo visivyosajiliwa, kuvisajili vituo hivyo ndani ya siku tisini kutoka leo. Baada ya hapo, ukaguzi wa kina utafanyika ili kuwabaini watakaoshindwa kutimiza vigezo vya kisheria ili wachukuliwe hatua ’’.


Sanjari na hilo amewataka maafisa ustawi  hao kuendelea kusuluhisha migogoro kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii na Ofisi za Ustawi wa Jamii ngazi za Halmashauri nchini. Ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023, jumla ya mashauri 28,773 yalipokelewa na kati ya hayo 22,844 yalifanyiwa usuluhishi katika Mabaraza ya Usuluhishi na Ofisi za Ustawi wa Jamii na 5,929 yalipewa rufaa kwenda mahamakani.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewaelekeza Maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini, kuendelea kutoa elimu ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii ili kupunguza au kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye makundi mbalimbali ya kijamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi