Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kwandikwa: Serikali Inaridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wa Tazara Fly Over
Oct 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_19483" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja mradi (TANROADS) Anold Maeda (wa tatu kushoto) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya TAZARA jana jijini Dar es Salaam.[/caption]

Na: Thobias Robert-MAELEZO

Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Ujenzi) Elias Kwandikwa amesema kuwa Serikali inaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa bababara ya juu (Fly Over) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la TAZARA.

Naibu Waziri huyo ameyabainisha hayo jana wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Oktoba na kuongeza kuwa serikali itazidi kuusimamia kwa karibu zaidi ili ukamilike kwa wakati.

“Ikumbukwe kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi alipotembelea mradi huu mwezi wa pili mwaka huu maendeleo ya ujenzi yalikuwa asilimia 25, lakini alipotembelea tena ujenzi wa mradi huu mwezi wa saba, mradi ulikuwa na ongezeko la asilimia 20 na kufikia asilimia 45, kuanzia mwezi wa saba hadi leo kuna ongezeko la asilimia 14 hivyo kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,” alifafanua Naibu Waziri Kwandikwa.

[caption id="attachment_19504" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (Katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja mradi (TANROADS) Anold Maeda (wa tatu kushoto) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya juu unaondelea katika makutano ya barabara ya TAZARA jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mhandisi Mkazi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Kiyokazu Tsuji.[/caption] [caption id="attachment_19489" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa mradi wa barabara ya juu (Fly Over) jana jijini Dar es Salaam.[/caption]

Aidha alisema kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa mradi huu ni njia ya kuimarisha uchumi na uzalishaji makazini kwani itasaidia kupunguza msongamano wa magari, pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma na bidhaa kutoka sehemu moja hadi nyingine.

“Watu wengi wamekuwa wakichelewa katika vituo vya kazi kama vile viwandani, maofisini na hata katika vituo vya umma, hivyo wamekuwa wakilipwa mishahara kwa kufanya kazi chini ya muda unaotakiwa, lakini pia tija katika shughuli za uzalishaji inapungua,  kwahiyo daraja hili litakapokamilika litawawezesha watu kuwahi kazini, maeneo ya uzalishaji pamoja na kutoa huduma kwa wakati, hivyo Fly over hii ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi,” alieleza Kwandikwa.

Aidha Naibu Waziri Kwandikwa alitoa wito kwa Mkandarasi kujenga kwa ufanisi, umakini na uimara ili kukamilisha mradi huo kwa kiwango na ubora wa hali ya juu utakaodumu kwa muda mrefu lakini pia wafanye kazi usiku na mchana ili wakamilishe mradi huu kwa wakati au hata kabla ya wakati uliopangwa.

[caption id="attachment_19492" align="aligncenter" width="750"] Meneja mradi (TANROADS) Anold Maeda (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati) kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Fly Over) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi huo jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mhandisi Mkazi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Kiyokazu Tsuji. (Picha na Eliphace Marwa)[/caption]

Kwa upande wake mhandisi anayesimamia ujenzi huo kutoka Japan, Kiyokazu Tsuji alieleza kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati kama ilivyosainiwa katika mkataba kwani wao wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Tazara Fly Over) ulianza rasmi mwaka 2015, ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2018. Mradi huu unajengwa kwa ufadhili wa Shirika la Kimtaifa la Maendeleo kutoka Japni (JICA) pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano utagharimu zaidi ya bilioni 94.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi