Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kushirikisha Taasisi za Umma katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la wizara katika Mji wa Serikali-Mtumba na hivyo kuziimarisha katika utoaji wa huduma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda ametoa pongezi hizo wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokagua ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati katika mji wa serikali, Mtumba jijini Dodoma tarehe 12 Machi, 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, Naibu wake, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Nishati walishiriki katika ukaguzi wa jengo hilo.
“Baada ya kufika hapa tumeona kuwa mkandarasi wa mradi huu ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mshauri Elekezi ni kampuni ya ABECC ambayo ipo chini ya Chuo Kikuu Ardhi, Kamati inawapongeza kwa hatua hii ya kuzishirikisha taasisi hizi za umma kwani pesa inayotolewa hapa na wizara inarudi kuiimarisha mihimili mingine ya Serikali.” Amesema Mhe. Ng’enda
Aidha, Mhe. Ng’enda amezitaka taasisi hizo zifanye kazi kwa kasi, weledi na kwa wakati ili kuwawezesha watumishi kuanza kutumia jengo hilo kutoa huduma kwa wananchi.
“Kwa kuwa mkandarasi umethibitisha kuwa fedha ya kutekeleza kazi hii unayo na unalipwa kwa wakati, hakikisha mnafanya kazi usiku na mchana na mhakikishe kuwa mafundi na vibarua wanalipwa pesa zao kwa wakati ili kuleta ufanisi kwenye kazi.” Amesema Mhe. Ng’enda
Vilevile, amemtaka mkandarasi kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika kwenye kazi ya umaliziaji wa jengo hilo vinapatikana kwa wakati ili kutochelewesha kazi nzuri ambayo imefanyika hadi sasa.
Awali, Msimamizi Kazi za Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati, Alphonce Kilovere alisema kuwa mradi huo umefikia asilimia 75 ambapo gharama ya mradi ni shilingi bilioni 25.2.
Aidha ameeleza kuwa, kazi ujenzi wa jengo hilo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.