Safari za Treni ya Umeme ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro zinatarajiwa kuanza Julai 2024 kama alivyoahidi Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alipozungumza na Waandishi wa Habari katika kambi ya ujenzi wa reli ya kisasa iliyopo wilayani Itigi, Mkoa wa Singida.
“Usafiri wa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro utaanza mwishoni mwa mwezi Julai kama alivyoelekeza Rais Samia Suluhu Hassan,” ameeleza Kadogosa.
Amearifu kuwa kwa sasa TRC inaendelea kujenga miundombinu ambapo ujenzi umefikia asilimia 99 akisema kuanza kwa safari kunategemea taasisi nyingine ikiwamo LATRA ambao ndio wanaopanga nauli za usafiri huu wa kisasa.
Pamoja na hilo, Kadogosa amefahamisha kuwa maandalizi ya majaribio ya treni hiyo ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma yanaendelea akieleza kuwa ujenzi wa miundombinu katika kipande cha Morogoro-Dodoma umefikia takriban asilimia 98.
TRC chini ya uongozi wa Masanja Kadogosa inaendelea na ujenzi wa kipande cha Makutupora-Tabora ambao umefikia asilimia 14 ambapo kuna kiwanda cha kuzalisha mataruma ya reli.