Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI  Yajipanga Kufanya Upasuaji  wa Moyo wa Kufungua Kifua na Kuwekewa Valvu kwa Wagonjwa 20
Sep 13, 2018
Na Msemaji Mkuu

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya  Misaada (IIRO) ya nchini Saudi  Arabia wanatarajia kufanya  upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na kubadilisha   valvu (milango ya moyo) zaidi ya miwili kwa wagonjwa 20.

Wagonjwa ambao wanabadilishiwa valvu na kuwekewa za bandia ni wale ambao valvu zao hazifanyi kazi vizuri na hivyo kuufanya moyo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.

Kambi hii ya siku saba ilianza tarehe  09/09/2018 na inatarajiwa kumalizika tarehe 15/09/2018 inaenda sambamba na utoaji wa elimu na kubadilishana ujuzi wa kazi  kati ya wafanyakazi wa Taasisi hizi mbili. Aidha wageni nao wamepata muda wa kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya  wa baadhi ya magonjwa ambayo katika nchi yao hakuna.

Tangu kuanza kwa kambi hii hadi jana   tarehe 12/09/2018 tumefanya  upasuaji na kubadilisha valvu kwa wagonjwa 11  ambao hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kutoka  katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kurudi wodini kwa ajili ya kuendelea na  matibabu ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi.

Kwa upande wa matumizi ya  damu wakati wa upasuaji mgonjwa mmoja  anatumia kati ya chupa tano  hadi saba lakini kama mgonjwa atapata tatizo anaweza kutumia chupa zaidi ya hizo. Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi  kuchangia damu ili wagonjwa wenye matatizo ya moyo waweze kufanyiwa upasuaji kwa wakati.

Aidha tunaendelea kuwasistiza wananchi  wajiunge na mifuko ya bima za afya wangali na afya njema wasisubiri kujiunga na mifuko hiyo wakati wagonjwa kwani gharama za matibabu hasa ya moyo ni kubwa na wakijiunga na mifuko hiyo  itawasaidia  kulipa gharama za matibabu pindi  watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.

Kwa namna ya kipekee tunaishukuru sana  Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya  Misaada (IIRO) kwa kutuma wataalam wake wa magonjwa ya moyo kuja hapa nchini kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wetu. Hakika Mwenyezi Mungu atawalipa kwa huduma hii mliyoitoa.

Hii ni mara ya pili kwa IIRO kuja kufanya kambi ya matibabu ya  moyo katika  Taasisi yetu. Kwa mara ya kwanza walikuja mwishoni mwa mwaka jana na kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono. Katika kambi hii jumla ya  wagonjwa 33 walipata matibabu.

Imetolewa na:

Kitengo cha Uhusiano

Taasisi ya  Moyo Jakaya Kikwete

13/09/2018

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi