Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Huduma za Ubingwa wa Juu BMH Zafikia 16
Mar 04, 2025
Huduma za Ubingwa wa Juu BMH Zafikia 16
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 4 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeboresha na kuongeza huduma za ubingwa wa juu kutoka 7 hadi 16 pamoja na huduma za kibingwa kutoka 14 hadi 20 ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora na gharama nafuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi ameyasema hayo leo Machi 04, 2025, katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.

Profesa Makubi amesema huduma za ubingwa zilizopo BMH kwa sasa zinajumuisha upandikizaji figo na matibabu yake, upandikizaji uloto, upasuaji wa mishipa ya damu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uvunjaji wa mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi na upandikizaji uume, upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu, upasuaji wa uti wa mgongo na kubadilisha nyonga na magoti.

Huduma zingine ni matibabu ya mfumo wa chakula, uchujaji damu, matibabu ya magonjwa ya moyo, uchunguzi na matibabu ya mishipa ya moyo kupitia maabara ya uchunguzi, uchunguzi na matibabu ya kiradiolojia, tiba ya magonjwa ya homoni na kisukari pamoja na huduma za upandikizaji mimba.

Akielezea baadhi ya huduma hizo, amesema katika kipindi cha miaka minne, BMH imefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 25, kupandikiza uloto kwa jumla ya watoto 20 waliokuwa na ugonjwa wa sikoseli, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua kwa wagonjwa 60, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa 1061 ambapo kati yao, upasuaji wa ubongo 771 na upasuaji wa uti wa mgongo 290 na huduma ya kuvunja mawe kwa kutumia mashine maalumu ya mawimbi kwa wagonjwa 504.

Pia, amesema kuwa BMH imefanikiwa kuweka vipandikizi kwa wanaume watano ambao walikuwa na changamoto za upungufu wa nguvu za kiume, uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya mfumo wa chakula kwa wagonjwa 10,000, kuanzisha na kutoa tiba ya magonjwa ya homoni na kisukari kwa wananchi 11,404 pamoja na kutoa tiba kwa wagonjwa wa saratani kwa kutumia tiba kemia ambapo wananchi 12,000 wamehudumiwa.

Kwa siku, Hospitali ya Benjamin Mkapa inahudumia wagonjwa wa nje 1000 hadi 1200 na wastani wa wagonjwa 250 hadi 300 wanalazwa huku ikielezwa kuwa katika kipindi cha miaka minne, jumla ya wagonjwa 972,740 wamehudumiwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi