Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hispania Yaonesha Nia Kusaidia Ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR
Sep 21, 2023
Hispania Yaonesha Nia Kusaidia Ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, yupo Madrid, Hispania, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara, na Utalii wa nchi hiyo, Bi. Xiana Mendez, ambapo Hispania, kupitia Wakala wake wa Bima (Export Credit Agency-ECA), imeonesha nia ya kushiriki katika mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kutoa mkopo, dhamana ya mikopo na Bima kwa kampuni za nchi hiyo zitakazojenga reli hiyo kuanzia Makutopora hadi Mwanza na Kipande cha kuanzia Tabora - Kigoma hadi Malagarasi, kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya nchi.
Na Benny Mwaipaja, Madrid, Spain

Hispania kupitia Wakala wake wa Bima (Export Credit Agency - ECA), imeonesha nia ya kushiriki katika mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kutoa mikopo, dhamana ya mikopo na Bima kwa kampuni za nchi hiyo zitakazojenga reli hiyo kuanzia Makutopora hadi Mwanza na Kipande cha kuanzia Tabora - Kigoma hadi Malagarasi, kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya nchi.


 

Ahadi hiyo imetolewa mjini Madrid, Hispania, na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara, na Utalii, Bi. Xiana Mendez, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ukiwemo ujenzi wa mradi huo mkubwa wa SGR.


 

Alisema kuwa Hispania inatambua umuhimu wa mradi huo kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi hiyo kwa kuwa kukamilika kwake kutaongeza mnyororo wa thamani wa uwekezaji na biashara na kuwa Kituo cha biashara katika Ukanda wa Afrika.


 

Bi. Mendez alisifu uchumi imara wa Tanzania pamoja na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji, hatua ambayo imezifanya kampuni nyingi kutoka nchi hiyo kutaka kushiriki katika uwekezaji na ujenzi wa miradi ya miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ikiwemo pia nishati jadidifu.


 

Aliahidi pia kuwa nchi yake itafungua Ofisi Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kurahisisha shughuli hizo za kibiashara.


 

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Hispania kupitia Wakala wake wa Bima, kwa kuonesha nia ya kuziwezesha kampuni za Hispania zitakazofanya shughuli zake za biashara na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini Tanzania, ukiwemo Mradi wa Reli,   mikopo, dhamana ya mikopo na Bima kwa kampuni zinazoshiriki katika ujenzi wa miradi nje ya nchi hiyo. 


 

“Ushiriki wa Wakala wa Bima wa Hispania (Export Credit Agency-ECA), katika kutekeleza mradi huo wa kimkakati ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na kwa ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya Hispania na Tanzania, na kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla” alisema Dkt. Nchemba.


 

Alisema kuwa katika kuimarisha uhusiano na maandalizi ya kutekeleza ufadhili huo wa SGR, Mkandarasi ametafuta kampuni 12 za Kihispania zitakazosambaza vifaa vitakavyotumika kujenga reli hiyo na kumwomba Naibu Waziri huyo na Serikali yake kwa ujumla, kuzishawishi kampuni nyingi zaidi kutoka nchini humo kujitokeza kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.


 

Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa mradi wa SGR ni muhimu kwa Tanzania kutokana na kuwa lango la biashara kwa nchi 7 za Ukanda wa Afrika na Maziwa Makuu zisizopakana na Bahari na kwamba utakapokamilika utachochea shughuli za biashara, usafiri na usafirishaji mizigo na hatimaye kuongeza pato la Taifa.


 

Aidha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Hispania kwa kufadhili ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo Mradi wa Umeme Vijijini (REA), maji, afya, usafirishaji, kilimo, pamoja na Shirika la maendeleo la nchini hiyo kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (FONPRODE), kuonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya Mradi wa Uendelezaji Bonde la Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam.


 

Zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.24 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha tatu, nne na cha tano kinachoanzia Makutopora hadi Mwanza, na ziara ya Mhe, Dkt Nchemba na ujumbe wake katika nchi za Ulaya ni kukutana na kufanya majadiliano na Taasisi za Fedha na wadau mbalimbali, kutafuta fedha za kugharamia ujenzi wa Reli hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi