[caption id="attachment_9378" align="aligncenter" width="340"] Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangalla. (Picha kutoka Maktaba)[/caption]
Na: Prisca Libaga, Maelezo -Arusha
Serikali Imeziagiza halmashauri zote nchini ambazo hazijakamilisha mpango wa taifa wa kutoa huduma ya vipimo kwenye Zahanati na Vituo vya Afya kuhakikisha vinakamilisha huduma hiyo ndani ya miezi mitatu kuanzia leo.
Agizo hilo limetolewa Leo na Naibu waziri wa afya, Dkt. Hamis Kigwangalla, katika ziara ya siku tano, kutembelea vituo vya Afya na Zahanati za Jiji la Arusha ili kuangalia utendaji na changamoto zilizopo katika kutekeleza agizo la uboreshaji wa huduma ya upimaji wa magonjwa. Amesema kuwa Rais Magufuli,alishatoa maelekezo ya kuimarishwa kwa huduma za Afya kuanzia ngazi za Zahanati na vituo vya Afya alipokuwa akifungua kikao cha Bunge mjini Dodoma,lengo ni kuokoa maisha ya wananchi ambapo wataweza kupata vipimo kwenye Zahanati na Vituo vya Afya.
Ameongeza kuwa Wizara katika kuhakikisha agizo hilo la rais linatekelezwa imetoa msisitizo wa utekelezaji huo pia hata Sera ya Wizara ya Afya inazitaka Halmashauri kuhakikisha huduma hiyo ya vipimo inapatikana kuanzia Zahanati hadi vituo vya Afya.,
Amesema kuwa rais aliagiza kuanzishwa kwa huduma ya upasuaji mdogo na vipimo kwa kuboresha kwa ujumla wake huduma hiyo kwenye ngazi za vituo vya Afya na Zahanati, lakini anashangazwa kuona Halmashauri ya Jiji la Arusha haijatekeleza kikamilifu maagizo ya rais. Amesema kuanzia sasa hataki kusikia mchakato wala mipango bali anataka aone utekelezaji wa maagizo ya rais na si vinginevyo.
Amesema wizara ya afya imeshatoa agizo la msisitizo wa utekelezaji wa maelekezo haya rais kwenye kikao kilichofanyika Mwandoya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu kusisitiza utolewaji wa huduma ya vipimo vya magonjwa kwenye Zahanati na vituo vya Afya na msisitizo ilikuwa ni kila Zahanati na kituo cha Afya lazima ziwe na maabara na vipimo vifanyike na hiyo itasaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali kubwa.
Amesema Wizara itazichukulia hatua halmashauri zote ambazo hazijatekeleza agizo la Wizara lililotolewa Mwandoya kwa kuwa kutokutekeleza ni uzembe ambao hauna nafasi serikalini na kuanzia sasa hakuna atakaye bakia salama iwapo ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
Waziri Kigwangalla, ametembelea vituo vya Afya na Zahanati mbalimbali za Jiji la Arusha na kukutana na changamoto mbalimbali.
Ikiwemo vituo na Zahanati kutokuwa na vyumba vya wajawazito kujifungulia wala kulaza wagonjwa na baadhi ya masine za kuchunguza magonjwa kutokufanya kazi.
Akaiagiza halmashauri ya Jiji la Arusha, inakusanya kodi ya shilingi bilioni 12 kwa mwaka halafu inashindwa kuboresha huduma ya Afya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Rebeka Mathias Mongi, amesema kuwa Halmashauri itakamilisha maelekezo hayo ndani ya muda uliotolewa na Waziri.Amesema kuwa huo utaanza mapema.