Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Filamu Mpya “Kisogo” ya Gabo Zigamba Sokoni
Jun 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Georgina Misama 

Kampuni ya Sarafu Media ikiongozwa na Mkurugenzi wake Salim Ahmed maarufu kwa jina la Gabo Zigamba imefanya uzinduzi wa filamu mpya ya kiswahili inayoitwa  “Kisogo” leo Jijini Dar es Salaam.

Akiongea na waandishi wa Habari katika uzinduzi wa filamu hiyo Gabo ambaye ana kipaji kikubwa cha kuigiza lakini pia ni mwongozaji wa filamu amesema kwamba filamu ya Kisogo imeandaliwa kitaalam, ikiwa na lengo kuu la kufanya mageuzi katika tasnia ya filamu nchini.

“Filamu ya Kisogo imelenga kutoa hamasa mpya kwa watanzania kuzipenda na kuzithamini filamu za kitanzania na zile za kiswahili hasa baada ya kujifunza kupitia makosa ambayo watanzania wamekuwa wakiyalalamikia katika filamu nyingi za kibongo” anasema Gabo Zigamba

Aidha, Gabo anasema kwamba kwa mara ya kwanza watanzania watafapa fursa ya kipekee na rafiki ya kuitazama filamu ya Kisogo pamoja nafilamu  nyingine zinazoandaliwa na kampuni ya sarafu kupitia simu ya kiganjani aina ya smati kwa kuzingatia kwamba idadi kubwa sasa ya watanzania wanamiliki simu hizo.

Akizungumzia gharama za upatikanaji wa filamu hiyo, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa kampuni ya sarafu media Mfwaisa Myovela amesema kwamba mtu yeyote ataweza kuangalia dakika 15 za filamu ya Kisogo bure na dakika 15 zilizobaki atachangia gharama kwa kiasi cha shilingi 500 na hivyo kukamilisha filamu hiyo fupi ya dakika 30.

“Filamu ya Kisogo tumeifanya iwe ya gharama ndogo ili watanzania wengi waweze kuiona. Lengo letu ni kufikisha ujumbe, na siku za usoni itafika mahali watanzania watapata nafasi ya kuzitazama filamu zetu bila kuchangia chochote” amesema Myovela

Jinsi ya kuifungua filamu hiyo kupitia simu ya kiganjani mtumiaji atalazimika kupakua mfumo wa uhondo, ambapo atajisajili au kwa kupitia mtandao wa kijamii wa facebook ama kwa kupitia barua pepe ya mhusika.

Filamu ya Kisogo imeshirikisha wasanii wakubwa katika tasnia ya filamu nchini wakiwemo Gabo Zigamba mwenyewe,  Wema Sepetu, Millard Ayo na wasanii wengine wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kuvaa uhusika na kufikisha ujumbe kwa jamii.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi