Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DRC Kongo Kujifunza Uongezaji Thamani Madini Tanzania
Sep 19, 2023
DRC Kongo Kujifunza Uongezaji Thamani Madini Tanzania
Afisa Biashara kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bw. Marcel Kasongo Yampanya akiwa na viongozi wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha wakizungumza wakati walipokuwa wakifanya ziara katika eneo la kituo hicho.
Na Na Mwandishi Wetu

Afisa Biashara kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bw. Marcel Kasongo Yampanya amewasilisha nia ya Serikali ya Kongo kuleta Vijana wengi nchini Tanzania kujifunza Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha.

Amebainisha  hayo  wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa kituo cha TGC baada ya kukitembelea  Septemba 19, 2023 katika ziara iliyolenga kujifunza na kuona namna ya kushirikiana na kituo hicho katika masuala ya Uongezaji Thamani Madini ya Vito  pamoja na kuhakikisha ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili katika kukuza sekta hiyo ndogo.

Ziara hiyo  inakuja wakati ambapo  nchi ya DRC Kongo imeonesha nia ya kukuza sekta ya madini ya vito na kuleta vijana wa Kongo kujifunza kutoka kwa wataalam  wa Tanzania ambao wamekuwa wakiongoza katika  utoaji wa mafunzo ya uongezaji thamani wa madini ya vito kwa upande wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Aidha, sehemu kubwa ya wakufunzi wa kituo hicho tayari wamepata utaalam wa shughuli hizo kutoka nchi mbalimbali zilizoendelea katika eneo hilo ikiwemo Thailand, India na China.

Aidha, ziara hiyo ya Afisa biashara wa Kongo imekuja ikiwa zimepita siku chache tu baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea shughuli za uongezaji thamani madini katika viwanda vikubwa vya kati na vidogo nchini Thailand ambapo shughuli hizo zimeshamiri kwa kiasi kikubwa ambapo katika ziara hiyo, Mratibu wa Kituo hicho pia alikuwa sehemu ya ujumbe huo.

Katika ziara ya hivi karibuni  nchini  Thailand, Wizara ya Madini kupitia kituo hicho ilifanya mazungumzo  na taasisi kadhaa kuhusu namna ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uongezaji thamani  ikiwemo kiwanda kikubwa chenye uzoefu wa miaka 50 katika shughuli za uongezaji thamani madini ambapo wadau nchini humo walifungua milango kwa watanzania  kujifunza ili kuwa bora katika eneo hilo.

Katika kikao hicho, Kaimu Mratibu wa TGC, Bw. Daniel Kidesheni amepokea ahadi ya Balozi na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya taasisi hizo mbili na kwamba amesisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kuendeleza teknolojia za kisasa ili kuhakikisha kuwa sekta  ndogo ya madini ya vito inachangia  katika ukuaji wa uchumi na maendeleo katika nchi hizo.

Wakati wa ziara hiyo,  Bw. Kasongo  amepata fursa ya kutembelea karakana mbalimbali za TGC, ikiwa ni pamoja na maabara za kisasa zinazotumika kwa uchunguzi wa madini ya vito, usonara na ukataji na ung’arishaji wa madini ya Vito.

Ziara hiyo ya Afisa biashara kutoka ubalozi wa DRC Kongo nchini Tanzania imekuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ndogo ya madini ya vito

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi