Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Biteko Awataka Wanawake Kuwa Mabalozi wa Nishati Safi ya Kupikia
Mar 04, 2025
Dkt. Biteko Awataka Wanawake Kuwa Mabalozi wa Nishati Safi ya Kupikia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza leo Machi 4, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme.
Na ONWM

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka wanawake kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia, ili kuhakikisha familia na jamii zote zinatumia nishati salama kwa afya na ustawi wa vizazi vijavyo.

Dkt. Biteko amebainisha hayo leo Machi 4, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme.

"Nimefahamishwa kuwa kongamano hili limeanza kwa mjadala mzito juu ya nafasi ya wanawake katika ajenda ya nishati safi ya kupikia ya umeme. Kupitia mijadala kama hii, tunaibua hoja muhimu na tunashirikiana na wadau wote muhimu kuweka mikakati ya kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034," amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amewataka kutumia vema fursa ya Maadhimisho ya Siku Kimataifa ya Mwanamke na kuwasihi wanawake wote kuibeba ajenda hiyo muhimu ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akiipa kipaumbele akiwa ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, kupitia Mfuko wa Nishati safi ya kupikia, Serikali itahakikisha kuwa wanawake wanapata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara za nishati safi.

Pia, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Sera na Sheria mbalimbali zinakuwa rafiki kwa wawekezaji wa nishati safi ya kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara ya nishati safi ya kupikia.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka Watanzania hususan wanawake kuendelea kuiunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima Nyamo - Hanga amesema kuwa Serikali imeweka msukumo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme kwa kuwa ni nafuu zaidi na imefika kila mahali nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi