Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DAWASA yaleta neema kwa wateja wake Jijini Dar es Salaam
Oct 12, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na; Mwandishi wetu

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea kuimarisha miundombinu yausambazaji maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kuchochea maendeleo  na ustawi wa wananchi.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imeeleza kuwa kazi ya kuunga mtandao mpya katika bomba la nchi 48 kutoka mtambo wa  Ruvu juu imekamilika hali itakayowawezesha wananchi wa Msigani,  Malamba, Mbezi kwa Yusuph, Temboni,  Goba,  Makabe na kwa Msuguri  kupata huduma ya maji ya  uhakika.

Faida za kupanua mtandao wa maji ni pamoja na kuwawezesha wananchi kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda vidogovidogo na kuongeza kasi katika shughuli za maendeleo kwa wananchi wa maeneo husika kama dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ilivyo.

“ Pampu za kusukuma maji katika mtambo wa Ruvu juu zimeshawashwa ili kusukuma maji  ili yawafikie wananchi katika maeneo husika ikiwa ni  muendelezo wa maboresho yanayofanywa na Mamlaka hiyo  yakilenga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora”; Inasisitiza sehemu ya taarifa hiyo

Mamlaka  hiyo imekuwa katika maboresho makubwa katika kuimarisha huduma zake ambapo inaendesha zoezi la kudhibiti uvujaji wa maji katika maeneo yote ya Jiji na tayari baadhi ya maeneo yaliyofikiwa ni pamoja na Tegeta na Magomeni Jijini Dar es Salaam.

Maboresho mengine ni pamoja na kuwepo kwa mifumo ya kielektroniki inayowawezesha wananchi kutoa taarifa za uvujaji wa maji au tatizo lolote linalowakabili ili Mamlaka hiyo iweze kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto husika kwa wakati ili kuongeza tija.

DAWASA  imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikiwemo kujenga miundo mbinu ya kisasa inayoendana na mahitaji ya wakati husika.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi