Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kutekeleza miradi mbambali ya maji ili kukidhi mahitaji ya maji lita bilioni 2.1 kwa siku ifikapo mwaka 2050 ikiwa ni makisio ya mara tatu ya mahitaji ya maji lita milioni 685 ya hivi sasa kwa siku.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire amesema hayo leo Machi 11, 2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Mhandisi Bwire ameeleza kuwa ni lazima kuwe na mipango ya muda mrefu ya kukidhi mahitaji ya maji ya maeneo yanayohudumiwa na DAWASA kwani kwa sasa ni mita za ujazo 685.6 lakini kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu pamoja na viwanda, mahitaji ya maji lazima yazingatiwe ndiyo maana DAWASA imeangalia mahitaji ya maji ya leo, ya miaka 10 ijayo, hadi ya mwaka 2050.
"DAWASA inatarajia mahitaji ya maji yataongezeka miaka kumi ijayo kufikia mara mbili ya mahitaji ya sasa na kufikia lita za ujazo milioni 1.2 kwa siku. Vile vile kufikia 2050, mahitaji ya maji yatafikia mara tatu ya sasa na kufikia mita za ujazo milioni 2.1. Ni vizuri tukaanza kufahamu haya kwani unapokuwa na makadirio haya lazima kuwe na mipango ya muda mrefu ya kuhakikisha DAWASA inakuwa na huduma ya maji itakayokidhi mahitaji", amesema Mhandisi Bwire.
Amefafanua kuwa, vyanzo vikubwa vya maji vilivyopo chini ya ardhi ni asilimia 7 na juu ya ardhi ni asilimia 93. Vyanzo vya juu ya ardhi ni mto Ruvu unaochangia asilimia 87, mto Wami unachangia asilimia 4 na Mtoni asilimia 2 ambapo vyanzo hivyo vinazalisha lita milioni 534.6.
Katika jitihada za kupunguza utegemezi wa maji juu ya ardhi, Mhandisi Bwire amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha maji chini ya ardhi yanapatikana ambapo imejikita katika kuchimba visima virefu zaidi ya mita 600 katika maeneo ya Kigamboni lengo likiwa ni kusaidia pale ambapo maji juu ya ardhi yanapokuwa na changamoto kuwe na mbadala wa upatikanaji wa maji.
Ametaja hatua ambazo serikali inazichukua kuhakikisha inafikia mahitaji ya maji yanayotakiwa ikiwemo; kuongeza visima ambavyo vina uwezo wa kuzalisha lita milioni 20 ambapo kufikia Juni, 2025 visima hivyo vitaongezewa uwezo na kuweza kuzalisha lita milioni 44 kutoka kwenye visima saba vilivyopo Kimbiji.
Pia, serikali itapanua mtambo wa Mtoni ili kuhakikisha unaweza kuzalisha lita milioni 12 kutoka lita milioni 9 kwa siku. Aidha, mtambo wa Ruvu chini utapanuliwa ili kuongeza lita milioni 90,000 kwa siku ili kuweza kuendana na mahitaji yanayoongezeka kwa kasi.
Vile vile, Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kutoa maji ya mto Rufiji na kuyaleta jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na DAWASA ambao upo kwenye hatua ya usanifu.