Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Balozi wa Indonesia, Rc Dodoma Wazungumza Utaratibu wa Kuhamishia Ofisi za Ubalozi Dodoma
Sep 19, 2023
Balozi wa Indonesia, Rc Dodoma Wazungumza Utaratibu wa Kuhamishia Ofisi za Ubalozi Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akimkaribisha mgeni wake Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Bw. Tri Yogo Jatmiko ofisini kwake jengo la Mkapa jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Bw. Tri Yogo Jatmiko pamoja na ujumbe wake, wamemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ofisini kwake leo Septemba 19 kuzungumza kuhusu utaratibu wa kuhamishia ofisi za Ubalozi huo kwenye Mji Mkuu wa Serikali Dodoma kwa lengo la kutekeleza agizo la Serikali la kuhamishia Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mazungumzo yao, Balozi Jatmiko amesema mwezi uliopita Rais wa Indonesia alikuja Tanzania na kuonana na Mhe. Rais Samia ambapo moja ya mambo waliyozungumza kubwa lilikua ni swali kutoka kwa Mhe. Rais Samia kuhusu lini Ubalozi wao utahamia Dodoma. Kufuatia mazungumzo ya viongozi hao, Mhe. Balozi ameamua kufunga safari hadi kwenye ofisi hii ili kupata utaratibu wa ujenzi wa ofisi za Ubalozi kutoka kwa mwenyeji wao Mhe. Senyamule.



Akitoa ufafanuzi juu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya Mabalozi wa nchi mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba, Mratibu wa Mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma, Bw. Meshack Bandawe, amesema kuwa Balozi zote zilizopo nchini zimetengewa maeneo maalumu na yenye ukubwa unaolingana wa heka 2.5 kwa eneo la ofisi na pia kuna maeneo kwa ajili ya makazi na watumishi wa Balozi hizo. Amewaonyesha ramani ya eneo lao ikiwemo majirani waliopakana nao ambao ni Ubalozi wa Burundi, Algeria, Namibia pamoja na Vietnam. Hata hivyo, amebainisha kuwa ujenzi wa Mji wa Serikali kwa sasa umefikia asilimia 70 hadi 80.



Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Senyamule, ameupongeza Ubalozi huo kwa kufuata taratibu za ujenzi wa ofisi za Ubalozi na kuhamia Dodoma kwakuwa ni wakati sahihi kwao kulingana na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa Dodoma ikiwemo uwanja wa ndege wa Msalato ambao utarahisisha shughuli za safari za kuingia na kutoka Dodoma. Pia amezungumzia ujenzi reli ya kisasa ya SGR ni miradi mingine ya kimkakati itakayorahisisha shughuli za kibalozi zitakapokua ndani ya Mkoa wa Dodoma.

Balozi Jitmiko amesisitiza kupatiwa nyaraka zitakazohusiana na eneo lao ili aweze kuziwasilisha kwa Waziri wao na kujadiliwa kwenye Bunge la Indonesia kwa ajili ya kupangwa bajeti ya ujenzi ili uweze kuanza mara moja. Pia Balozi huyo amesema Indonesia ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya kiteknolojia ikiwemo kwenye sekta za madini na umeme kwani wana teknolojia za kisasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi