Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

WCF Yasajili Waajiri 13,500.

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kupata mafanikio ya kusajili waajiri 13,500 na kulipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 2.52 hadi kufikia tarehe 28 Februari 2018.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Jenista Mhagama kwenye mkutano baina ya waajiri walio wanachama wa chama cha waajiri (ATE) na taasisi ya sekta binafsi tanzania (TPSF) kanda ya kati pamoja na watendaji wa serikali na WCF.

“Katika kuhakikisha uendelevu wa Mfuko, utoaji wa huduma bora na malipo stahiki ya fidia, Mfuko pia umekuwa ukiwekeza kwenye vitega uchumi mbalimbali kwa kufuata kanuni na miongozo ya serikali ili kuhakikisha uwekezaji salama na wenye tija, ambapo  katika kipindi cha Mwaka 2016/2017 Mfuko ulipata shilingi bilioni 10.4 kama mapato yanayotokana na uwekezaji” ameeleza Waziri Jenista.

Aidha, Waziri Jenista amesema kuwa, Serikali ilianzisha Mfuko huu wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata mafao bora ya fidia tofauti na Sheria ya zamani ya Fidia kwa Wafanyakazi.

“Kwa mfano, kwa mujibu wa Sheria ya zamani, viwango vya juu vya malipo ya fidia ilikuwa ni shilingi 108,000 kwa mfanyakazi anayepata ajali kazini au shilingi 83,000kwa mfanyakazi anayefariki kwa ajali ama ugonjwa kutokana na kazi anayoifanya kwa mujibu wa mkataba wa ajira yake” amesema Waziri Jenista.

Akizungumzia kuhusu faida za Mfuko huo, Waziri Jenista amesema kuwa Mfuko huu una faida kubwa kwa Wafanyakazi, Waajiri, na Taifa kwa ujumla kwani hivi sasa wafanyakazi wanauhakika wa kinga ya kipato kutokana na majanga yasababishwayo na ajali, magonjwa au vifo kutokana na kazi.

Mbali na hayo Waziri Jenista, amebainisha baadhi ya changamoto zinazoukumba mfuko huo ni pamoja na Mfumo wa viwango vya malipo ya uchangiaji unaolalamikiwa na baadhi ya wadau ambapo sekta ya Umma inachangia asilimia 0.5% ya mshahara wa mfanyakazi na sekta Binafsi inachangia asilimia 1% ya mshahara wa mfanyakazi bila kuzingatia kiwango cha vihatarishi katika sekta husika.

“Changamoto nyingine ni baadhi ya waajiri kutojisajili na kuchangia kwenye Mfuko, uelewa mdogo wa wadau kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, waajiri kutowasilisha kwa wakati nyaraka muhimu ili kuwezesha Mfuko kufanya tathmini na kulipa fidia” ameongeza Waziri Jenista.

Hata hivyo Waziri Jenista amesisitiza kuwa, mkutano huo ni sehemu ya utekezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara Tanzania ya kuhakikisha Serikali inakuwa sikivu na kuzifanyia kazi changamoto za wadau kupitia majadiliano ya pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama