Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mbarawa Atembelea Miradi ya Maji Mpanda Vijijini na Mlele

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa na Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Katavi, Anna Lupembe kwenye kisima cha maji cha Itenka B katika Halmashauri ya Nsimbo, mkoani Katavi.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ametembelea Wilaya za Mpanda Vijijini na Mlele, mkoani Katavi kukagua maendeleo ya miradi ya maji ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Profesa Mbarawa amekagua miradi ya maji ya Itenka B katika Halmashauri ya Nsimbo katika Wilaya ya Mpanda Vijijini, Kashishi na Chamalendi katika Halmashauri ya Mpimbwe katika Wilaya ya Mlele.

Akiwa katika miradi hiyo Profesa Mbarawa amewaonya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo; Kampuni za Hematech Investment Ltd (Itenka B), Dan General Construction Ltd (Kashishi) na Monmars and Sons Ltd (Chamalendi) kuwa hakuna sababu ya miradi hiyo kuendelea kuchelewa kukamilika kwa kuwa hakuna tatizo la fedha kwa Serikali na kila hati ya malipo watakayoipeleka wizarani italipwa.

Amesema wanachotakiwa ni kufanya kazi usiku na mchana kwa kuzingatia weledi, uaminifu na viwango vya ubora kwa vifaa vyote vya ujenzi, mabomba ya maji, kutimiza taratibu zote na makubaliano ya mkataba;kwa kuwa hatakubaliana na visingizio vyovote na hatasita kuwafutia usajili wanaoleta ubabaishaji kwenye miradi ya maji.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye kituo cha maji cha mradi wa Kashishi, Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

‘‘Hali ya huduma ya maji kwenye Halmashauri ya Nsimbo ni asilimia 40, ndio maana Serikali imetoa Shilingi Milioni 371 kwa ajili ya ujenzi wa mradi katika Kijiji cha Itenka B chenye kata sita kwa nia ya kuwasaidia wananchi hawa kupata huduma ya maji.Vilevile, nataka Kijiji cha Itenka A nao wafikiwe na huduma ya majisafi na salama mara baada ya kukamilika kwa mradi huu’’, aliagiza Profesa Mbarawa.

‘‘Nataka mkandarasi ukamilishe mradi huu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu ili wananchi waanze kupata maji, kwa kuwa ulitakiwa kufanya hivyo mwezi Agosti. Kwa hiyo sitakuvumilia tena ukishindwa kufanya hivyo, zaidi ya kukufutia usajili kwenye Bodi ya Wakandarasi na usahau kutapata kazi nyingine tena’’, alionya Profesa Mbarawa.

Akiwa kwenye mradi wa Chamalendi, Profesa Mbarawa hakuridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuionya Kampuni ya Monmars& Sons Ltd yenye kandarasi ya ujenzi wa mradi huo, naendapo haitakamilisha mradi huo kwa wakati hatasita kuvunja mkataba nao na kutafuta mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kukamilisha mradi huo.

‘‘Sitakubaliana na wakandarasi wababaishaji kwa sababu wananchi hawa wana haki ya kupata maji na sio visingizio vyovote vile. Ule ubabaishaji wa miaka ya nyuma hauna nafasi kwa Serikali ya sasa, kama mkandarasi hana uwezo asiombe kazi Tanzania kwa sababu hatapewa kamwe’’, alisisitiza Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amesema ataendelea kuzunguka mikoa yote nchini kukagua kila mradi, ili kuhakikisha anasukuma kasi ya utekelezaji miradi yote na kutimiza lengo la Serikali ifikapo mwaka 2020 hali ya huduma ya maji mjini kufikia asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

140 thoughts on “Mbarawa Atembelea Miradi ya Maji Mpanda Vijijini na Mlele

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama