Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Makamba Aongoza Kampeni ya Upandaji Miti Katika Mji wa Serikali

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali kutoka kwa Mhandisi Simeo Machibya ambae ni Meneja Msimamizi wa Mradi kutoka Vikosi vya Ujenzi. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.  January Makamba hii leo ameongoza watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kupanda miti zaidi ya elfu moja (1000) katika eneo la Mji wa Serikali, inapojengwa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri Makamba amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu na takribani miti 1000 ya aina ya mdodoma inayostahimili ukame imepandwa hii leo. “Sisi ni watu wa Mazingira, ni lazima tuonyeshe mfano, hapa kila mtumishi atakuwa na wajibu wa kutunza miti atakayokabidhiwa na kuhakikisha inakua” Makamba alisisitiza.

Waziri Makamba amesema kuwa Jiji la Dodoma linakabiliwa na changamoto ya mandhari kutokana na ardhi yake kuwa kame na kupelekea uoto wa asili kupungua kwa kiasi kikubwa. Hivyo, ametoa wito kwa kila taasisi na Idara kuunga mkono kwa vitendo kampeni iliyozinduliwa na Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 2017 ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, kwa kupanda miti kwa wingi katika Mji wa Serikali na Dodoma kwa ujumla ili uwe mji wa mfano kwa kuwa na mandhari yakuvutia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizindua zoezi la upandaji miti katika mji wa Serikali Dodoma. Miti 800 aina ya “midodoma” imepandwa katika eneo hilo na miti 200 ya aina nyingine pia imepandwa ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Kulia ni Bw. Timothy Mande Afisa Misitu kutoka Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais.

“Kwa kuwa sisi ndio wasimamizi wa Mazingira, upandaji na usimamizi  wa miti ni sehemu ya Hifadhi ya Mazingira, hivyo lengo la Ofisi yetu ni kuonyesha mfano, watumishi wote kuanzia Waziri mpaka Mhudumu kila mmoja atakuwa na miti yake ya kutunza na kuhakikisha inakua” Makamba alisisitiza.

Awali Waziri Makamba alipata fursa ya kutembelea eneo inapojengwa Ofisi ya Makamu wa Rais na kuridhishwa na kasi ya ujenzi katika eneo hilo na kumtaka Mkandarasi wa Mradi kutoka (Vikosi vya Ujenzi) Mhandisi Simeo Machibya kukamilisha kazi yote kwa wakati. “Ujenzi huu ufanyike usiku na mchana” Makamba alisisitiza.

Katika zoezi la leo Waziri Makamba ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo, Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali.

 

78 thoughts on “Waziri Makamba Aongoza Kampeni ya Upandaji Miti Katika Mji wa Serikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama