Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Magembe Apiga Marufuku Minada ya Ng’ombe Hifadhini.

Na Tiganya Vincent – RS Tabora

Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe amepiga marufuku minada ya ng’ombe wanaokamatwa katika Misitu ya Hifadhi kufanyika katika maeneo hayo badala yake ifanyike katika maeneo ya wazi ili kutoa  nafasi kwa wananchi kushiriki kwa uwazi.

Waziri Magembe alisema hayo juzi mjini Kahama katika ziara yake wilayani kahama kufuatia oparesheni za kuondoa mifugo kwenye Misitu ya Hifadhi ambapo mifugo hiyo imekuwa ikipigwa mnada ndani ya hifadhi badala ya maeneo ya wazi.

Kwa mujibu wa waziri Magembe utaratibu huo wa kuendesha minada ndani ya Misitu ya Hifadhi umekuwa ukiwanyima nafasi wananchi pamoja na wamiliki wa mifugo hiyo kushiriki katika zoezi hilo.

Profesa Maghembe alisema kuwa kabla ya mnada kufanyika ni vema Mkuu wa Wilaya husika afahamishwe ili yeye na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama iwepo wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo ili kuondoa manung’uniko kutoka kwa wenye mifugo na wananchi.

Waziri huyo aliongeza kuwa ni vema kabla ya siku ya mnada kufanyika, Mkurugenzi Mtendaji ataarifiwe ili awatangazie wananchi wote katika eneo lake kwa ajili ya kushiriki mnada hatua itakayoondoa malalamiko.

Naye Meneja wa Pori la Akiba la Moyowosi, Kigosi Patrick Kutondolana alisema kuwa hifadhi hiyo inakabiliwa na tatizo la kuwepo kwa kundi kubwa la ng’ombe kutoka nchi za jirani ambazo mwanya huo kuwinda wanyamapori kinyume cha sheria.

Alisema kuwa tatizo jingine ni wananchi wanaopewa vibali vya kulina asali badala yake wamekuwa wakitumia vibali hivyo kuendesha shughuli za ujangili na kuwinda wanyama mbalimbali huku wakiwa wameficha silaha zao.

Meneja huyo aliongeza kuwa wakimbizi kutoka Kambi ya Nduta mkoani Kigoma wamekuwa wakiingia katika Hifadhi hiyo na kuendesha shughuli za ujangili kwa kutumia silaha za kivita ambazo wametoka nazo makao kisha kurudi makambini.

Waziri Maghembe alikuwa na ziara katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Geita na Kagera kwa ajili ya kuangalia zoezi la uondoaji wa watu waliovamia katika maeneo mbalimbali ya Hifadhi.

 

 

 

82 thoughts on “Waziri Magembe Apiga Marufuku Minada ya Ng’ombe Hifadhini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama