Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Kalemani Aviwashia Umeme Vijiji Vingine Zaidi

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe, kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Kijiji cha Nyijundu, Wilaya ya Nyang’hwale, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, jana Septemba 17, 2018. Kulia kwake (mwenye kofia) ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel na kushoto kwake ni Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kassu.

Na Veronica Simba – Geita

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasha umeme katika vijiji kadhaa vya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita na Kwimba mkoani Mwanza; hivyo kuendelea kuongeza idadi ya vijiji vyenye umeme nchini.

Alifanya kazi hiyo jana, Septemba 17, 2018 akiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, alipofika kumweleza nia ya ziara yake mkoani humo; Waziri Kalemani alisema kuwa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, unatarajiwa kusambaza umeme kwenye vijiji na vitongoji zaidi ya 220 pamoja na kuunganisha wateja wapatao 12,944.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kanegele, Wilaya ya Nyang’hwale, Mkoa wa Geita, jana Septemba 17, 2018; katika hafla ya uwashaji rasmi wa umeme kijijini hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza, wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na wananchi wa Kijiji cha Nyijundu, jana Septemba 17, 2018. Waziri Kalemani aliwasha rasmi umeme katika Kijiji hicho.

Aidha, alisema kuwa; kukamilika kwa Mradi husika, kutafanya Mkoa wa Geita kuwa na ongezeko la asilimia 45 ya wateja, kutoka 28,483 waliopo sasa hadi kufikia idadi ya wateja 41,427 hapo mwakani.

Akifafanua zaidi kuhusu faida za Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 2019, Waziri alisema kuwa, utafanya jumla ya vijiji 372 kati ya 499 vilivyopo kuwa na nishati ya umeme, ambavyo vitakuwa ni asilimia 75 ya vijiji vyote vya Mkoa wa Geita.

“Matarajio yetu ni kuwa, mzunguko wa pili wa Mradi, unaotegemewa kuanza Julai 2019, utamalizia vijiji vilivyobaki na kufanya vijiji vyote vya Mkoa wa Geita kuwa na nishati ya umeme kwa asilimia 100,” alisema.

Akizungumzia kuhusu Wilaya ya Nyang’hwale ambako alifanya ziara na kuwasha umeme katika vijiji vya Kanegele na Nyijundu, Waziri Kalemani alieleza kuwa, mzunguko wa kwanza wa Mradi utapeleka huduma ya umeme kwenye vijiji 30 ambapo jumla ya wateja 1,288 wataunganishwa.

Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kassu, akizungumza, wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na wananchi wa Kijiji cha Nyijundu, jana Septemba 17, 2018. Waziri Kalemani aliwasha rasmi umeme katika Kijiji hicho.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel, mbali ya kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo; aliwataka wananchi kutambua kuwa maendeleo hayaji kwa siku moja, bali ni hatua kwa hatua.

Akifafanua kuhusu kauli yake, Mhandisi Gabriel alieleza kuwa, anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kwamba wangependa kuona vijiji vyote vinapatiwa nishati hiyo kwa mkupuo. Hata hivyo, aliwataka waiamini Serikali yao kuwa itahakikisha vijiji vyote nchini vinapatiwa umeme, kazi inayofanyika hatua kwa hatua.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme katika moja ya nyumba za wakazi wa Kijiji cha Kanegele, Wilaya ya Nyang’hwale, Mkoa wa Geita, kuashiria uwashaji rasmi wau meme katika eneo hilo, jana Septemba 17, 2018.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia), akimkabidhi Kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kissu kwa ajili ya kuwagawia wananchi wa Kijiji cha Kanegele, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wau meme kijijini hapo, jana Septemba 17, 2018. Waziri alitoa jumla ya vifaa hivyo 20 bure kama motisha kwa wananchi ili wachangamkie huduma ya kuunganishiwa umeme.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kassu, aliipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwapelekea wananchi wa Jimbo lake, hususan walioko vijijini nishati ya umeme.

Aliiomba Serikali iendeleze jitihada zaidi ili kuwafikishia huduma hiyo muhimu wananchi wote hivyo kuwezesha maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani pia alitembelea Kijiji cha Sanga kilichopo wilayani Kwimba, Mkoa wa Mwanza, ambako aliwasha rasmi umeme katika eneo hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uwashaji umeme, Waziri alisema kwamba Serikali imedhamiria kupeleka umeme katika vitongoji vyote 137 vya Wilaya hiyo; vikiwemo vitongoji vyote Tisa vya Kijiji cha Sanga.

Waziri Kalemani anaendelea na ziara yake ya kazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

Sehemu ya umati wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyang’hwale wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipowatembelea na kuwasha rasmi umeme katika vijiji vya Kanegele na Nyijundu akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, jana Septemba 17, 2018.

 (Picha zote na Veronica Simba – Wizara ya Nishati)

 

155 thoughts on “Waziri Kalemani Aviwashia Umeme Vijiji Vingine Zaidi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama