Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Kalemani Aagiza Waliolipia Umeme Kuunganishiwa Kabla ya Mwaka Kuisha.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibaga, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wakati wa ziara yake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Na Veronica Simba.

Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wateja wote walioomba na kulipia huduma hiyo mwaka 2017 wanaunganishiwa kabla ya Desemba 30 mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Singida na Dodoma.

“Agizo hili ni kwa nchi nzima. Hakikisheni wateja waliowasilisha maombi yao na kulipia ndani ya mwaka huu wa 2017 wawe wameunganishiwa umeme siyo zaidi ya Desemba 30 mwaka huu.”

Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa shirika hilo kutoa elimu kwa umma, hasa wananchi walioko vijijini kuhusu umuhimu wa kutumia umeme ili kuwahamasisha kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto), akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, jimboni kwake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Akifafanua, Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati hiyo katika maeneo yao.

“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa kutumia umeme hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali walipo, hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.

Akizungumzia faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.

Aliongeza kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe, ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiwakabidhi baadhi ya wazee kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutandaza mfumo wa nyaya kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili – kushoto) na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto) wakimsikiliza Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Ngozi kilichopo kijiji cha Idifu, Wilaya ya Chamwino, Dkt. Francis Njau (wa tatu – kulia), kuhusu mahitaji ya umeme kwa kiwanda hicho.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Idifu, Wilaya ya Chamwino alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Waziri aliwapongeza viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge na Watendaji wa Halmashauri na Vijiji, kwa jitihada zao za kufuatilia utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi ikiwemo upelekaji wa umeme vijijini.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutunza miundombinu ya umeme katika maeneo yao ili isihujumiwe na hivyo kuwakosesha huduma hiyo muhimu na pia kuleta hasara kwa serikali.

Ziara hiyo ya Waziri Kalemani ni muendelezo wa ziara mbalimbali ambazo amekuwa akifanya nchi nzima kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupokea kero na changamoto mbalimbali za wananchi kuhusu sekta ya nishati ili zifanyiwe kazi.

Katika ziara hii, Waziri ametembelea Wilaya za Mkalama na Singida  Vijijini mkoani Singida pamoja na Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

 

119 thoughts on “Waziri Kalemani Aagiza Waliolipia Umeme Kuunganishiwa Kabla ya Mwaka Kuisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama