Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Hasunga Abainisha Jitihada za Serikali Katika Mapinduzi ya Kilimo

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo – Dar es salaam

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuweka mazingira bora ya kuleta mapinduzi katika kilimo.

Japokuwa Kilimo kinachangia karibu asilimia 30 ya Pato la Taifa, ukuaji wa Sekta ya Kilimo bado hauridhishi kutokana na changamoto zilizopo, japo kumekuwepo na mwelekeo chanya katika siku za karibuni. Kulingana na taarifa zilizopo za hivi karibuni ukuaji wa sekta ya kilimo umefikia asilimia 7.1

Waziri wa Kilimo, Japhet  Hasunga ameyasema hayo leo Februari 21, 2019 wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania – Dar es salaam.

Alisema kuwa kwa kutambua hilo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) kwa kushirikiana na wadau wa sekta inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).

Lengo kuu la ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.

Alisema kuwa utekelezaji wa lengo hilo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula,kuimarisha uchumi, kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda, na kuongeza ajira.Ili kufikia malengo haya; utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Alizitaja jitihada zingine katika kuleta mapinduzi ya kilimo ambazo ni kuanzishwa kwa eneo maalum la kuboresha mnyororo wa thamani kwa mazao mbalimbali, kuanzishwa kwa Program ya Miundo Mbinu ya Masoko, uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) ambao lengo lake kuu ni kusaidia nyanja mbalimbali muhimu katika kuendeleza kilimo cha kisasa nchini na kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo (yaani TADB) ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima na shughuli za kilimo nchini.

Alisema kuwa jitihada za dhati zinahitajika kuwashawishi vijana kwa njia mbalimbali ili nao waingie katika biashara ya kilimo hasa katika uboreshaji wa mnyororo wa thamani kutokea shambani hadi kwa mlaji.

Kuwepo kwa huduma kama bima ya afya kwa wakulima na makazi bora kunaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kuwafanya watu wengi zaidi haswa vijana kujihusisha na kilimo kwa njia za kisasa zaidi na usalama wa afya zao na makazi yao pia.

Allisema kuwa hiyo itakuwa njia bora ya kutatua mahitaji yao na kuwasaidia wakulima vijana kufanya shughuli za kilimo pamoja na kilimo biashara kwa ufanisi. “Umefika wakati sasa tuhamasishe kuwa na Kilimo cha mashamba makubwa na ya kati yatakayopelekea kuzalisha kwa wingi na kwa tija” Alikaririwa Mhe Hasunga.

Mkutano huo utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 21 Februari 2019 mpaka kesho tarehe 22 Februari 2019 ukiwa na lengo la kujadili namna bora ya kuwajengea wakulima uwezo wa kustahimili matukio mbalimbali kwa kutumia huduma za fedha vijijini, namna ya kuwanufaisha wakulima na huduma za hifadhi ya jamii, bima ya afya, matumizi ya teknologia rafiki ya kuwafikishia huduma za fedha vijijini, makazi bora kwa wakulima pamoja na elimu ya fedha vijijini.

Mkutano huo umewajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo maafisa kutoka serikalini, watoa huduma za kifedha vijijini, wataalam wa mambo ya kifedha, wakulima, na wawakilishi wa mashirika.

 

96 thoughts on “Waziri Hasunga Abainisha Jitihada za Serikali Katika Mapinduzi ya Kilimo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama