Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Zaidi ya shilingi Milioni 800 zahitajika kuendesha Mashindano UMISETA na UMITASHUMTA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene (aliyesimama mbele) akiongea na wadau toka Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA 24 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.

Na Husna Saidi-MAELEZO.

Katika kuendesheza michezo mbalimbali nchini ikiwemo mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISETA) pamoja na Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA), zaidi ya shilingi milioni 800 zinahitajika katika kuendesha mashindano hayo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene wakati wa hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya michezo hiyo.

Waziri Simbachawene alisema kwamba, Serikali ina jukumu la kuendesha michezo shuleni katika shule za msingi na sekondari ili kutafuta vipaji vya vijana mbalimbali ambao wataweza kuliwakilisha Taifa na kuongeza vipato vyao kwa manufaa yao na familia zao.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyekaa mbele kulia) akiwashukuru wadau mbalimbali toka Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi wakati wa uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA 24 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa wadau toka Kampuni ya Sportpesa akiongea jambo na kutoa ahadi ya uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA kwa niaba ya Kampuni 24 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.

Aidha. Alisema kuwa kwa sasa Serikali inakusudia kuendesha mashindano hayo kuanzia ngazi za shule za msingi na sekondari kwani huko ndiko vipaji vingi vinakopatikana.

“Kuna shule mbalimbali za michezo zinaendelea kuendesha michezo kwa wanafunzi na ndizo zinasaidia kuibua vipaji mbalimbali vya vijana, hivyo kuna haja ya kukuza vipaji kwa vijana wetu kupitia shule wanazosoma”, alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, baadhi ya changamoto zinazokwamisha mashindano ya michezo ni pamoja na ufinyu wa viwanja vya mazoezi, fedha kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali vinavyotumika na wanamichezo kwani baadhi ya vifaa hivyo vinauzwa kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewaeleza wadau wa michezo nchini juu ya umuhimu wa mashindano hayo ambapo amesema kwamba, kuna haja ya kuisadia sekta ya michezo na kuthamini vipaji vya vijana nchini ili waweze kuliletea sifa Taifa.

Dkt. Mwakyembe alisema kuna baadhi ya vijana ambao wanavipaji vikubwa katika michezo mbalimbali hususani mpira wa miguu, hivyo vijana hao wanatakiwa kupewa hamasa ili waweze kujituma zaidi.

“Mashindano haya ya UMISETA na UMITASHUMTA yatasaidia kuibua vipaji mbalimbali vya vijana wetu kwani kuna vijana wengi ambao vipaji vyao vimejificha na wanajua michezo mbalimbali”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Wadau walioshiriki hafla hiyo ni 13 ambapo kati yao walitoa shilingi milioni 30 huku wadau wengine wakitoa ahadi ya kuchangia mashindano hayo.

Mashindano hayo kwa mwaka huu yanatarajiwa kushirikisha jumla ya Mikoa 28 ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania Visiwani inatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali toka Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi wakati wa hafla ya uchangiaji fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA 24 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama