Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watumiaji Mitandao ya Kijamii Walaumiwa Kudhalilisha Wanawake

Mjumbe wa Sekretarieti toka Taasisi ya Ulingo wa Wanawake Bi. Saum Rashid akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitoa karipio juu udhalilishaji wa wanawake katika mitandao kwa kisingizio cha siasa, katikati ni Bi. Angelina Mutahiwa na kulia ni Bi. Dominata Rwechungura wajumbe wa Sekretarieti hiyo.

Na: Thobias Robert

Taasisi isiyo ya kiserikali inayoundwa na Jumuiya za Wanawake wa Vyama vyote vya siasa (Ulingo) imelaani vitendo vya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya viongozi wanawake wana siasa pamoja na serikali kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Saum Rashid alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwaaajili ya kulaani watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wanawake.

Mjumbe wa Sekretarieti toka Taasisi ya Ulingo wa Wanawake Bi. Angelina Mutahiwa akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitoa karipio juu udhalilishaji wa wanawake katika mitandao kwa kisingizio cha siasa, kushoto ni Bi. Saum Rashid na kulia Bi. Dominata Rwechungura wajumbe wa Sekretarieti hiyo.

“Matusi ambayo wanatupiwa na watu wasio na maadili ni matusi siyo kwa wahusika tu bali kwa wanawake wote, hivyo ikumbukwe kuwa hao wanaowalenga wanafamilia, watoto na marafiki na wanaongoza mamilioni ya watanzania,” alifafanua Bi. Saum.

Akizungumza bila kuwataja wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kudhalilisha viongozi, Bi.Saum alisema wanawake wanapodhalilishwa hasa na wanawake wenzao inawakatisha tamaa katika kutimiza majukumu yao hivyo akaomba mamlaka husika kusimamia Sheria ili mitandao isitumike vibaya.

Aidha Bi. Saum amesema kuwa anaamini viongozi wanawake ambao wamepewa heshima na dhamana ya kuongoza, wana uwezo mkubwa na wanastahili kuwa kwenye nafasi walizo nazo .

Mjumbe wa Sekretarieti toka Taasisi ya Ulingo wa Wanawake Bi. Dominata Rwechungura akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitoa karipio juu udhalilishaji wa wanawake katika mitandao kwa kisingizio cha siasa, katikati ni Bi. Angelina Mutahiwa na kushoto ni Bi. Saum Rashid wajumbe wa Sekretarieti hiyo.

Baadhi ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Mjumbe wa Sekretarieti toka Taasisi ya Ulingo wa Wanawake Bi. Angelina Mutahiwa (aliyekaa katikati) wakati wakitoa karipio juu udhalilishaji wa wanawake katika mitandao kwa kisingizio cha siasa. (Picha na Eliphace Marwa)

Taasisi hiyo ambayo inawashirikisha pia watu wenye ulemavu imelaani vikali vitendo vya udhalilishaji na kuwataka watanzania warejee kwenye misingi ya utu na kuthaminiana kama maadili ya kitanzania yanavyoelekeza hasa kwa watoto wa kike.

Kwa upande wake Angelina Mutahiwa ambaye pia ni Mjumbe wa taasisi ya Ulingo alisema kuwa, mwanamke ni mlezi mzuri wa maadili katika jamii hivyo kumdhalilisha ni kuvunja malezi na maadili katika jamii na kuchochea vitendo viovu dhidi yake ambavyo vitadumu kizazi hadi kizazi.

 “Wale wachache ambao wameonesha utovu wa nidhamu kwa kuendelea kumnyanyasa mwanamke watambue kwamba wao hawapo juu ya sheria na katiba ya nchi iko wazi hairuhusu mwanamke kudhalilishwa, kuonewa wala kufanyiwa vitendo vya kikatili haikubaliki na hatutakubali,” alisistiza  Bi.Mutahiwa.

Ulingo ni taasisi isiyo ya kiserikali inayoundwa na jumuiya za wanawake wa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kwenye na Msajili wa vyama vya siasa hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja mmbalimbali ili waingie kwenye vyombo vya maamuzi.

Taasisi hiyo kwa sasa inapigania haki sawa kwa wanawake yaani 50/50 kwani waaamini kuwa uongozi ni haki ya kila mtu kwa maana ya wanawake na wanaume.

87 thoughts on “Watumiaji Mitandao ya Kijamii Walaumiwa Kudhalilisha Wanawake

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama