Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watendaji wa Serikali Watakiwa Kuzingatia Mwongozo wa Bajeti

Na Fatma Salum – MAELEZO

Serikali imewaagiza watendaji wakuu na viongozi wote Serikalini kuzingatia kikamilifu mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya mwaka 2018/2019 ili uweze kuleta tija na kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akitoa hutuba ya kuahirisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Majaliwa aliagiza kuwa watendaji hao ambao ndio maafisa masuuli katika taasisi zao wahakikishe wanazingatia mambo yote muhimu yaliyoainishwa kwenye mwongozo ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti.

Alibainisha kuwa miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo aliwataka maafisa masuuli kuhakikisha makusanyo yote yanawekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

“Maafisa masuuli waendelee kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya uendeshaji wa taasisi zao ili kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha taasisi zinazojiendesha kibiashara zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu,” alisema Majaliwa.

Katika kudhibiti matumizi na kupunguza gharama, Majaliwa aliwataka waendelee kufanya uhakiki wa watumishi ili mishahara ilipwe kwa watumishi wanaostahili, wanaopaswa kupandishwa madaraja wahakikiwe na malimbikizo yote ya madeni yabainishwe ili yaweze kulipwa.

Aidha, Majaliwa aliwaagiza maafisa masuuli hao kuhakikisha madai ya watoa huduma wote yanahakikiwa na mkaguzi mkuu wa ndani wa hesabu za Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika.

“Serikali inawataka kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha pamoja na kuzingatia matumizi ya hati za ununuzi zinazotolewa kwenye mfumo wa malipo ili kudhibiti malimbikizo ya madai,” alisisitiza Majaliwa.

Nao wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wametakiwa kuzingatia miongozo inayotolewa na kuwashirikisha wananchi pamoja na wadau wa sekta binafsi katika kupanga mipango ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Pia Majaliwa aliagiza Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha kazi ya kuandaa mwongozo wa maandalizi wa mpango wa bajeti na kuusambaza kwa wadau wote ili taasisi zote za umma zianze mchakato wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2018/2019.

6,517 thoughts on “Watendaji wa Serikali Watakiwa Kuzingatia Mwongozo wa Bajeti