Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watanzania Tunzeni Mazingira, Askofu Gadi.

Mwenyekiti wa Kanisa la Good News For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi (katikati) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akifanya maombi maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu wa kanisa hilo Mchungaji Palemo Massawe na kushoto ni Mchungaji wa kanisa hiliAndrew Thomas.

Na. Neema Mathias.

Askofu wa kanisa la Good News For All, Dkt. Charles Gadi ametoa wito kwa wananchi na serikali kuyatunza mazingira na uoto wa asili ili kuchangia uwepo wa hali nzuri ya hewa.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Askofu Gadi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo aliongoza maombi maalum kwa lengo la kuombea  tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa  juu ya uwezekano wa kutokea kwa upungufu mkubwa wa mvua za vuli katika mikoa mingi hapa nchini.

Askofu Gadi amesema kuwa wananchi wote wanapaswa kulinda mazingira  ikiwemo kupiga vita ukataji ovyo wa miti na badala yake wapande miti kwa bidii ili kuilinda mazingira kutokana na uharibifu unaosababisha ukame unaotokana na ukosefu wa mvua.

Mwenyekiti wa Kanisa la Good News For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi (wa pili toka kulia) pamoja na wachungaji wa kanisa hilo wakifanya maombi maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo jijini Dar es Salaam.

 Aidha askofu huyo amesema kuwa wao kama viongozi wa dini wanakubaliana na utabiri wa kisayansi uliotolewa ambao mara nyingi umekuwa ukifanikiwa, lakini haitokuwa sawa kusubiri hadi hali hiyo ya ukame itakapotokea wakati Mungu amewapa Imani na mamlaka ya kuomba dhidi ya majanga kama hayo.

“Good News for All kwa kushirikiana na madhehebu mbalimbali tumekuwa tukiendesha mikutano ya kuiombea nchi dhidi ya ukame tangu mwaka 2006 ambapo ni zaidi ya miaka 11 sasa tunamshukuru na Mungu amekuwa akijibu maombi yetu,” alisema Askofu Gadi.

Pia, Askofu Gadi amesema kuwa kutokana na uzoefu walionao wanatoa wito kwa viongozi wengine wa dini kufanya maombi ili ukame huo usitokee.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kanisa la Good News For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi wakati akifanya maombi maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo jijini Dar es Salaam.Picha na Eliphace Marwa.

“Ukame ni jambo baya kwa uchumi, ni baya kwa afya ya watu na baya kwa viumbe hai wote wakiwemo wanyama na mimea hivyo tuungane kwa pamoja katika kuliombea jambo hili,” alifafanua Askofu Gadi.

Aidha, Askofu gadi amesema “jambo la kufurahisha ni kwamba mvua ni hazina nzuri ya Mungu, tena ndicho kitu cha thamani ambacho alikiacha duniani kwaajili ya kuendesha uhai aliouumba hususani kwa viumbe hai.

Vilevile Askofu Gadi amefafanua kuwa maandiko matakatifu katika Biblia yanaonyesha kuwa mvua ni mali ya Mungu na ameahidi pasipo shaka kwamba tukimwomba atatupatia, ndiyo maana wana Imani na ujasiri kuomba dhidi ya ukame na majanga mengine kila mara na Mungu amekuwa mwaminifu kwa neno lake kwa kujibu maombi.

“Katika kitabu cha Matendo ya mitume 14:17, lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha,” alieleza Askofu Gadi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama