Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wanawake Kufanya Kongamano Kumuombea Rais Magufuli

Na. Thobias Robert – MAELEZO

Wanawake wa Jumuiya ya Tanzania Fellowship of Churches kutoka makanisa mbalimbali wanatarajia kufanya kongamano la maombi na dua maalumu kwa ajili ya kumuombea ulinzi Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika kutetea wanyonge na kulinda rasilimali za nchi.

 Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa kongamano hilo Mchungaji Deborah Malassy, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo la siku tatu linalotarajia  kuanza Julai 20 hadi Julai 23 mwaka huu katika ukumbi wa  Millenium Tower ulioko Jijini Dar es Salaam.

Mchungaji Malassy alisema kuwa, kongamano hilo linalenga kutoa shukrani kwa Mungu kwa kuipatia nchi ya Tanzania kiongozi ambaye Watanzania walikuwa wanamhitaji kwa muda mrefu ili kulinda amani ya nchi, kutetea wanyonge pamoja na kusimamia rasilimali za nchi pamoja na uadilifu kazini.

“Mwaka huu ni mwaka wa baraka na neema kwa Taifa la Tanzania kufuatia matendo makuu ya Mungu aliyotutendea Watanzania, hasa kuwa na kiongozi mwenye uwezo, mcha Mungu, mtiifu mkweli na asiyependa mapato ya Serikali kupotea,” alisema Mchungaji Malassy.

Aidha alieleza, kwa muda mfupi aliokaa madarakani, Rais Magufuli amefanya mambo mengi na kila Mtanzania ameyashuhudia kama vile kurejesha maadili kwa watumishi wa Umma, kuwaondoa viongozi wala rushwa pamoja na kutetea rasilimali za Tanzania zilizokuwa zikisafirishwa nje ya nchi, mfano mchanga wa dhahabu.

Vile vile kongamano hilo litatoa elimu kwa wanawake juu ya  kujilinda dhidi ya unyasasaji wa kijinsia, na kuwajengea Wanawake uwezo wa namna ya kujikwamua kiuchumi pamoja na kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia unaotokana na rushwa ya ngono.

Akinukuu Maneno ya kitabu kitakatifu kutoka kitabu cha Nyakati wa Pili 7:18, Mchungaji Malassy alisema, “Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu wataziacha njia zao mbaya wakajinyenyekesha na kuomba nami nitasikia kutoka mbinguni na nitaiponya nchi yao,” kwahiyo wao kama wakina mama walioitwa kulia na kuomboleza kwa ajili ya Taifa lao wanayo haki ya kufunga na kuomboleza kwaajili ya kuliombea Taifa.

Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Vile vile, viongozi wanawake kutoka nchi za Afrika ya Kusini, Marekani, Uingereza, Zambia, Kenya, Kongo na Botswana pia watakuwepo katika kongamano hilo.

 Kongamano hilo limekuwa likifanyika kila mwaka mwezi Julai na Disemba ambapo hufanyika pamoja na mkesha mkubwa wa maombi katika uwanja wa Taifa, lengo likiwa ni  kuombea amani, utulivu, upendo pamoja na kuwaombea viongozi wa Serikali ili waongoze Nchi kwa hekima na busara kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

23 thoughts on “Wanawake Kufanya Kongamano Kumuombea Rais Magufuli

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama