Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wachimbaji Igunga Watakiwa Kuondoa Tofauti Zao

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) alipofanya ziara kwenye machimbo yaliyopo Igurubi Wilayani Igunga. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Manonga lilipopo wilayani humo, Seif Gulamali.

Serikali imewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini wenye migogoro kukaa chini kujadili na kuondoa tofauti zao ili kuwa na uchimbaji unaokusudiwa.

Naibu Waziri wa Madini Stansalus Nyongo alitoa wito huo juzi alipofanya ziara kwenye maeneo ya Machimbo ya Dhahabu kwenye Tarafa ya Igurubi wilayani Igunga na kujionea shughuli zilizokuwa zikiendelea na kuzungumza na wachimbaji.

Wachimbaji hao walimueleza Nyongo changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo migogoro baina yao ambayo walisema inasababisha shughuli za uchimbaji kuzorota na hivyo kuwakosesha kipato.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akitembelea maeneo ya Machimbo ya Dhahabu ya Igurubi, Wilayani Igunga.

Walimuomba Naibu waziri Nyongo kuingilia kati kukomesha migongano iliyopo baina yao ili waendeleze maeneo hayo.

“Mheshimiwa Waziri kama unavyotuona, tumekaa tu, hawa wamiliki wa haya machimbo wapo kwenye migogoro na hivyo tumeagizwa kuacha kuendelea na shughuli yoyote hapa,” alisema Alfred Mateo ambaye ni miongoni mwa wachimbaji waliomueleza Naibu Waziri changamoto zinazowakabili.

Naibu Waziri Nyongo aliwaagiza wenye machimbo hayo kukaa pamoja kutazama namna ya kuondoa tofauti zao ili shughuli za uchimbaji kwenye maeneo hayo zifanyike ili wao na wachimbaji wajipatie  kipato na wakati huohuo Serikali ikipata mapato yake kutokana na uchimbaji.

“Nyinyi mnavyoendelea kuzozana na kusimamisha uchimbaji watu wengi waliopo hapa wanaathirika, ninaona kuna wananchi wengi maeneo haya wamekuja kufanya kazi lakini hawana kazi kwa sababu ya migogoro yenu,” alisema.

Aliiagiza Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Tabora, kuhakikisha anaratibu mazungumzo baina ya wachimbaji wenye migogoro na apatiwe taarifa ya makubaliano yatakayofikiwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akitembelea maeneo ya Machimbo ya Dhahabu ya Igurubi, Wilayani Igunga.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akitembelea maeneo ya Machimbo ya Dhahabu ya Igurubi, Wilayani Igunga.

Aidha, Nyongo alizungumzia wananchi wanaohodhi maeneo mengi bila ya kuyafanyia kazi ambapo alisema Tume ya Madini itakapoanza kazi, maeneo hayo yatatazamwa na kugawiwa upya kwa wananchi wenye nia ya dhati ya kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji.

Alisema leseni nyingi zimekwisha muda wake ipo haja ya kurudisha leseni hizo kwa Serikali ili izigawe upya kwa wananchi wenye uhitaji wa maeneo ya uchimbaji.

“Wapo wajanja wachache wanamiliki leseni nyingi wakisubiri wawekezaji, hawa tutawanyang’anya ili wananchi wapate maeneo kwani hawaziendelezi,” alisema.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha migodi inatoa ajira kwa wananchi mbalimbali wakiwemo wa maeneo yenye migodi na kwamba kutoendeleza migodi hiyo kunasababisha ajira nyingi kupotea hali ambayo alisema Serikali haiwezi kuifumbia macho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama