Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waandishi Wa Habari Kupewa Vitambulisho Bila Kujali Ngazi Zao Kielimu

Na Adelina JohnBosco – MAELEZO

DODOMA.

Serikali imeahidi kutoa vitambulisho kwa waandishi wote wa habari nchini kuanzia wenye ngazi ya cheti ‘astashahada’ na kuendelea ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma, Mkurugezi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amesema serikali imechukua uamuzi huo ili kuwawezesha waandishi wenye taaluma ya habari kuanzia ngazi ya chini kuweza kutambulika katika shughuli zote za kukusanya na kusambaza habari.

“Utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari unaendelea na wakati wowote kuanzia sasa tutaunda Bodi ya Ithibati ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kusajili wanahabari na kuwapa vitambulisho vya kitaaluma na kusimamia maadili yao”, amesema Dkt. Abbasi.

Licha ya kitambulisho kumwezesha mwandishi kupata taarifa kwa urahisi, pia kitamsaidia kutambulika na kumlinda mwandishi awapo katika kazi yake ameeleza Dkt. Abbasi.

Aidha, amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kukuza sekta ya habari kwa kurahisisha mchakato wa kutoa na kupata taarifa ambazo zitawafikia wananchi wengi. Ikumbukwe Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa haki ya kukusanya na kusambaza taarifa.

Mbali ya kuwahakikishia mazingira rafiki ya utendaji kazi kwa wanahabari wenye vitambulisho, vilevile, ametoa rai ya kuchangamkia fursa za kujiendeleza kitaaluma ambazo zinatarajiwa kutolewa na serikali siku za usoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama