Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Uzalendo na Maadili Ndiyo Nguzo ya Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda.

Na: Thobias Robert

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imeanza kurejea katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere juu ya uchumi wa viwanda aliouanzisha ili kukidhi matarajio ya wananchi ambayo ni kuzalisha bidhaa zitokanazo na malighafi za hapa nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Akizindua  Kongamano la kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika  Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere  jijini Dar es Salaam, Ole Nasha alisema kuwa Mwalimu Nyerere alijenga viwanda vingi hapa nchini vikiwemo, viwanda vya nguo kama  Urafiki, Mbeya Tex, Mwatex, Mutex, viwanda vya ngozi, viwanda vya zana za kilimo, viwanda vya kutengeneza vipuli, pamoja na viwanda vinavyotegemea malighafi za mazao yanayolimwa hapa nchini  kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wananchi kuliko kutegemea uagizaji wa bidhaa kutoka mataifa ya nje.

Aidha alisema kuwa, taifa linahitaji viongozi wazalendo na waadilifu kama alivyo Rais Magufuli ambaye ameonyesha nia ya dhati ya kufuata nyendo za mwalimu Nyerere kwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea viwanda.

“Serikali ya awamu ya tano kwa muda wa miaka miwili iliyokaa madarakani imejitahidi kurejea na kuweka kwenye vitendo dhana ya Mwalimu Nyerere ya uchumi wa viwanda, kwani  kwa sasa  inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa, mwaka  2016/2017-2020/2021 unayojikita katika ujenzi wa viwanda kama njia ya maendeleo ya kiuchumi na maisha ya watu.” Alieleza Waziri Ole Nasha.

Aliendelea kusema kuwa mtazamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kutumia viwanda vya ndani kama njia ya kujinasua kutoka kwenye unyonyaji wa muda mrefu ambao nchi maskini kama Tanzania zilikuwa zinafanyiwa na nchi tajiri na zenye maendeleo makubwa ya viwanda. Nyerere alipinga tabia ya nchi kuendeshwa  kwa kutegemea bidhaa zinazozalishwa kutoka nje ya nchi.

Kama Taifa huru kuna haja ya kuondoa tofauti za kisiasa na kuishi katika misingi ya usawa, umoja, ushirikiano ili kujiletea maendeleo ya uchumi kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla ikiwemo kuhimiza uzalendo kwa kila mtanzania ili kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila alieleza kuwa ili kufikia Tanzania ya viwanda taifa linahitaji viongozi wazalendo wenye uchu wa maendeleo na wasio na misingi ya ukabila, udini na wenye nidhamu ya kiuongozi kama walivyokuwa viongozi wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, hivyo ustawi wa uchumi wa viwanda  unahitaji viongozi na watendaji ambao ni wazalendo, watiifu na wenye kutanguliza mbele maslahi ya taifa,” alifafanua Prof. Mwakalila.

Kongamano la maadhimisho ya siku ya  Mwalimu Nyarere hufanyika kila mwaka ili kujadili busara, fikra na hekima zake katika kujenga usawa, maendeleo, umoja na ustawi wa uchumi wa taifa letu. Kongamano la mwaka huu linahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na siasa pamoja na wasomi ambapo mada mbalimbali kuhusu mwalimu Nyerere zinawasilishwa  kwa ajili ya kuchangia na kujadiliana.

Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 18, tangu Mwalimu Nyerere afariki mnamo tarehe 14, Oktoba, 1999, ambapo kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu inasema “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.Maadhimisho hayo yatafanyika visiwani Zanzibar ambapo shughuli ya kuzima mwenge wa hururu itafanyika.

 

 

 

 

2 thoughts on “Uzalendo na Maadili Ndiyo Nguzo ya Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama