Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tumedhamiria, Tunachapakazi, Tunatekeleza

Barabara ya Bagamoyo -Makofia – Msata yenye urefu wa Kilomita 64 imekamilika.

Na Dkt. Hassan Abbasi*

WIKI iliyopita katika utangulizi wa safu hii muhimu inayowaunganisha wananchi na Serikali yao kujua mikakati iliyopo na utekelezaji wake, nilianza kwa kuchambua, kama nchi, tunataka kwenda wapi. Tuliangalia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Katika makala hiyo tuliona jinsi Dira hiyo inavyosisitiza misingi mikuu kama ya kuwa na Taifa lenye watu walioelimika, uchumi imara, amani na utulivu, utawala bora na maisha bora kwa kila Mtanzania.

Niliahidi kuwa leo na makala kadhaa zijazo za wasemaji wengine wa Serikali kupitia wizara, taasisi na hata mikoa, tutaanza kuonesha namna maono haya ya Dira yalivyofafanuliwa kiutekelezaji katika malengo yanayopimika, kuwekewa mikakati na kutekelezwa.

Ni kwa minajili hiyo basi, makala yangu ya lengo inalenga kuchokoza tu mada na kisha kuanzia wiki ijayo tutaanza kusoma watekelezaji wenyewe mahsusi katika kila eneo wanasema nini kuhusu kinachoendelea katika maeneo yao. Hapa nitapitia kwa ujumla tuko wapi katika kila eneo la Dira.

Maisha bora

Katika misingi mikuu ya Dira tuliona kuwa imelenga kuona Tanzania inaboresha maisha ya watu wake, kuhakikisha wanakuwa na kipato kizuri lakini pia kuwe na mgawanyo mzuri wa kipato kitakachoboresha maisha ya Watanzania.

Dira inasema: “Kwa Tanzania dhana ya maendeleo ni kwamba kila kipato kinachopatikana basi kutawanyike kwa haki kwa kila mwananchi na usiwe na vikwazo vya kitaba au kijinsia katika kufaidi matunda hayo.”

Kwanza kwa ujumla wake Serikali imefanyakazi kubwa tangu uhuru, licha ya changamoto za uchanga wa Taifa, kutokuwepo wataalamu wa kutosha (tulikuwa na madaktari nane tu na wahandisi wawili mwaka 1961), hali ya uchumi duniani na changamoto nyingine.

Barabara nyingi zinaendelea kujengwa na kuboreshwa. Leo unaweza kutoka Kusini Mashariki hadi Kaskazini Magharibi mwa nchi ukiwa katika barabara za lami tupu. Serikali imenunua ndege mpya mbili na tayari nyingine ziko kiwandani. Ujenzi wa reli ya kisasa umeanza.

Huduma za jamii kama maji, umeme na afya (leo tuna madaktari zaidi ya 2,190) zinaendelea kuimaishwa mwaka hadi mwaka na hapa unavyosoma makala haya vijiji vinaunganishiwa umeme, miradi ya maji inatekelezwa mijini na vijijini kwa lengo la kuhakikisha Mtanzania anakuwa na maisha mazuri na changamoto za usambazaji wa dawa zinamalizwa.

Upo mfano wa mafanikio katika sekta ya maji. Kwa mfano takwimu za Wizara zinaonesha kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu idadi ya wananchi wanaopata maji vijijini imeongezeka kutoka chini ya asilimia 50 miaka kadhaa nyuma hadi asilimia 72. Wizara inalenga kufikia asilimia 100 katika miaka mitatu ijayo.

Eneo hili ni pana na linagusa masuala mengi ya maisha ya wananchi ndio maana naona tuwape fursa wasemaji wenyewe wa maeneo husika katika makala zijazo watueleze kwa kila na kila eneo nini kimefanyika na nini bado katika kufikia azma ya Dira.

Utawala Bora

Tumeeleza katika makala iliyopita kuwa utawala bora ni msingi wa maendeleo kwa sababu pasipokuwa na misingi ya kisheria, utii wa sheria, utoaji wa haki kwa wananchi hata lengo la kwanza la dira kama tulivyoliona hapo juu halitafikiwa. Ndio maana Dira inasisitiza kuwa msingi wa utawala wa sheria uwekewe mikakati madhubuti.

Utekelezaji wa falsafa ya utawala bora nchini uko imara kwa sababu tunayo mihimili ya dola inayotekeleza kazi zake ipasavyo, tunazosheria mbalimbali ambazo zimetungwa kusimamia haki za watu na Serikali pia, imekwenda mbali, kwa kuridhia mikataba ya kimataifa ili kuwe na uwajibikaji wa kimataifa pia.

Ujenzi wa utawala bora unaweza kutazamwa na kupimwa kwa namna nyingi. Ipo pia misingi ya kidemokrasia ambayo nchi yetu inaienzi kama vile kufanya uchaguzi mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba, kuruhusu vyama vingi, uhuru mkubwa wa habari ambapo leo tuna magazeti 430 yaliyosajiliwa, vituo 32 vya televisheni na redio 148.

Lakini pia taasisi muhimu kama Tume ya Uchaguzi, Bunge, Mahakama, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma vinafanyakazi. Zaidi nchi yetu, kuonesha inavyojiamini, ni miongoni mwa nchi 35 za Afrika zilizojiunga na Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) lakini pia ni miongoni mwa nchi chache zilizoridhia kushtakiwa na raia wake kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Uchumi Imara

Tuliona katika makala ya awali kuwa hatuwezi kuzungumzia amani na utawala bora kama nyenzo za kuwaletea wananchi maendceleo bila kuwekwa misingi imara ya kukuza uchumi ili kuwapatia wananchi maendeleo. Uchumi imara huzaa Taifa imara na ndio msingi mkuu wa kuifikia “Tanzania yenye neema.”

Dira imeliona hili na inasisitiza: “Tanzania inapaswa kuwa na uchumi imara na unaotegemea sekta nyingi ambao unaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kimaendeleo na kuhimili mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia.”

Kutoka harakati ngumu za ujenzi wa misingi ya Taifa (national building project), kusaidia uhuru kwingineko Afrika (liberation struggle) hadi mageuzi ya kiuchumi (economic liberalization) miaka ya 1990, uchumi wa Tanzania umeendelea kutoka mchanga hadi imara kiasi.

Katika mwaka 2016 uchumi wa nchi ulikua kwa wastani wa asilimia 7.0 kutokana na kukua na mchango wa sekta mbalimbali kama mawasiliano, ujenzi, madini, uzalishaji viwandani na biashara. Hadi Machi, mfumuko wa bei ulikuwa katika asilimia 6.4 ambayo ni chini ya ukomo wa asilimia 8.0 uliowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika mwaka 2016/17, sera za mapato zililenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 17,798.10 (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa). Hadi Aprili, 2017 mwaka huu jumla ya makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa) yalikuwa shilingi bilioni 13,604.0 sawa na asilimia 76 ya makadirio.

Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 11,644.6 sawa na asilimia 77 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 15,105.1; mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,600.8 sawa na asilimia 79 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 2,027.6; na mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 398.7 sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 665.4 kwa mwaka. Kufikia Juni 30 mwaka huu malengo nayatarajiwa kufikiwa na hata kuvukwa.

Amani na Usalama

Unaweza kuwa na uchumi imara na ila kitu katika Taifa lakini kukosekana kwa usalama na amani kunaweza uathiri yote tena ndani ya usiku mmoja. Tanzania imekuwa nchi ya amani ikilinganishwa na mataifa mengi Afria na duniani. Amani hii ni johari ya thamani.

Dira yetu imebaini hilo na imesisitiza kuwa amani na usalama wa raia na mali zao na Taifa kwa ujumla vinapaswa kujengwa, kuendelezwa na kulindwa kwa kiwango cha juu kabisa. Dira katika hili inasema:

“Ingawa Tanzania imekuwa na amani na umoja wa kitaifa, tunu hizi ni lazima ziendelee kuenziwa, kuimarishwa na kuendelezwa kama nguzo kuu za kufikia malengo ya Dira hii.”

Serikali imeanzisha vyombo mbalimbali vya dola katika kuhakikisha nchi inakuwa salama. Vyombo hivi vimefanyakazi kubwa na vinaendelea kutekeleza majukumu yao kwa kujituma sana kwa niaba ya nchi hii.

Watu Walioelimika

Katika hili hakuna anayeweza kubishana kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na ndio msingi mkuu wa mafanikio ya mwanadamu katika jitihada zake za kukabiliana na changamoto za kimaisha. Kwa kuona umuhimu huu kuwa na Taifa lenye watu walioelimika na kupata stadi muhimu za kiufundi ni muhimu sana.

Dira inasema: “Kuwa na watu wenye mawazo ya kimaendeleo ni muhimu lakini huwezi kuwa na watu hao bila elimu. Tanzania itajibariki yenyewe iwapo itahakikisha inakuwa na raia wenye ujuzi, ubunifu ili kuhimili ushindani.”

Katika eneo hili Dira inasisitiza Serikali kuweka mikakati ya kuwa na si tu raia walioelimika lakini pia wenye mtazamo chanya katika kuipenda nchi yao, kuchukia maovu, kufanyakazi kwa bidii, wanaojiamini na wenye kuheshimu mawazo ya wengine.

Serikali imechukua hatua nyingi na madhubuti katika kufikia azma hii. Tunapozungumza muda huu elimu yetu kutoka awali mpaka kidato cha nne ni bure kwa maana Serikali inatoa ruzuku katika sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji na hakuna ada.

Vyuo Vikuu nako mfumo wa mikopo umesaidia kusomesha maelfu ya wananfunzi katika vyuo vya umma na binafsi. Nchi yetu leo ina vyuo vikuu vya umma pamoja na vituo na kampasi zake vipatazo 19 na vyuo binafsi na kampasi na shule zake vipatavyo  41 (kwa mujibu wa Kamisheni ya Vyuo Vikuu nchini, TCU). Vijana wengi wanapewa pia mafunzo ya ujasiriamali na uzalendo katika kufikia kuwa walinzi madhubuti wa Taifa hili.

Baada ya utangulizi wangu huu sasa kuanzia wiki ijayo siku kama ya leo na mahali hapa hapa usikose maelezo murua kutoka wizara mbalimbali kueleza walipofikia. Tutaanza na Wizara ya Nishati na Madini.

Alamsiki.

*Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali. Anapatikana kwa baruapepe: mih@habari.go.tz.

 

One thought on “Tumedhamiria, Tunachapakazi, Tunatekeleza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama