Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TFF kuanza kuchapisha taarifa ya mapato na matumizi ya fedha kwenye magazeti

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiteta na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Michael Wambura (kushoto) baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa TFF uliofanyika leo katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.

Na Genofeva Matemu.

Uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umetakiwa kufikia Januari mwakani kuwajibika kama mashirika mengine ya mpira wa miguu duniani yanavyowajibika kuchapisha taarifa ya mapato na matumizi kwenye magazeti ili wananchi wapate fursa ya kufahamu namna fedha zinavyopatikana na jinsi zinavyotumika katika kuboresha  na kuendeleza usimamizi bora wa soka nchini.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo  Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na leo katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma

Aidha Mhe. Mwakyembe amewapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne kwa kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwapongeza washiriki wote waliothubutu kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi Mkuu wa TFF wa mwaka huu.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Wallace Karia (kulia) akiapa mbele ya Wakili na Msajili wa Vyama vya Michezo nchini Bw. Ibrahimu Mkwawa (aliyesimama kushoto) baada ya kutangaza mshindi wa nafasi hiyo leo katika Ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.

Mwakilishi wa TFF kutoka zoni namba nne Bi. Sarah Chao (kulia) akiweka sahihi katika kiapo alichoapa baada ya kutangaza mshindi leo wakati wa Mkutano Mkuu wa TFF Mkoani Dodoma. Kushoto aliyesimama ni Wakili na Msajili wa Vyama vya Michezo nchini Bw. Ibrahimu Mkwawa

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya hiyo Pro. Elisante Ole Gabriel (katikati) wakifuatilia uapisho wa viongozi wapya wa TFF waliochagulia leo katika Mkutano Mkuu wa TFF Mkoani Dodoma.

Kwa upande wake Rais mpya wa TFF Bw. Wallace Karia amewaahidi wapiga kuwa wake kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwani nafasi aliyopewa na wajumbe hao kwa kumuamini ni deni ambalo atalilipa kwa kuleta mafanikio makubwa katika mchezo wa soka.

Bw. Karia amesema kuwa furaha waliyonayo viongozi wote waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne iende kuwa furaha ya kazi kwa kufanya yale watanzania wanatarajia kutoka kwao.

 

ev eşyası depolama