Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TEWUTA Wampongeza JPM Suala la Airtel

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) Bw. Junus Ndaro (katikati) akieleza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu pongezi zao kwa Rais wa Jamhuri Muugano Magufuli juu ya suala la Kampuni ya Simu ya Airtel, kulia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Pius Mkuke na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Chrysostom Gapiti.

Na. Paschal Dotto.

Chama cha wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano (TEWUTA) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  kwa agizo la kuitaka kampuni ya simu ya Airtel kuanza kuchunguzwa.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam,  Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Junus Ndaro alisema kuwa chama hicho kimefurahishwa na uamuzi wa Rais Magufuli la kutaka kutatua suala hilo ambalo wamelilalamikia kwa mda mrefu.

Bw. Junus amesema kuwa uamuzi huo umewagusa Watanzania walio wengi hasa wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwani imekuwa faraja kubwa kwao kwa kuleta matumaini mapya kwa kushudia kampuni yao iliyoanzishwa kwa mtaji na jasho lao ikirejeshwa na kuwa mali ya Umma baada ya kuporwa bila aibu na viongozi waliokuwa hawana uzalendo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) Bw. Pius Mkuke (katikati) akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu suala la Kampuni ya Simu ya Airtel, kulia ni Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Junus Ndaro, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Chrysostom Gapiti. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam,(Picha na Paschal Dotto).

“TEWUTA kupitia kumbukumbu zetu za chama kwa miaka mingi tangu 2005 tuliwasilisha malalamiko yetu kufuatia kuporwa kwa kampuni ya simu Tanzania lakini malalamiko hayakupata majibu, tunamshukuru kwa dhati Rais Magufuli kuamua kufuatilia hili”, alisema Junus Ndaro.

Amesisitiza kuwa kulikuwepo na mchezo mchafu uliosababishwa na watanzania wachache wenye uchu wa fedha na wasiojali maslahi ya nchi yao waliosaidiana na wawekezajia katika kupora rasilimali hii muhimu kwa Taifa.

Aidha, chama hicho kinampongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya simu Tanzania, Mhandisi Omary Nundu kwa kuwa tayari kuthibitisha uhalali wa kampuni ya simu ya Airtel.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Pius Makuke alisema kuwa TTCL haikupora kampuni ya Airtel pekee bali ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu kitendo ambacho kilisababisha wafanyakazi wake kukosa mahali sahihi kwa kupata mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma

“Mbali na pongezi hizo, tunazidi kuisisitiza Serikali kukamilisha mchakato wa uchunguzi juu ya taarifa hizo pamoja na kufuatilia undani na kuzirejesha mali zote za kampuni ya simu Tanzania zilizoporwa kifisadi katika kipindi cha ubinafsishwaji wake ikiwemo kilichokuwa Chuo cha Posta na Simu kilichopo kijitonyama jijini Dar es Salaam”, alisema Makuke.

TTCL ilibinafsishwa kwa mwekezaji wa nje mnamo mwaka 2001, wakati huo kampuni hiyo ilikuwa imeshaanzisha kampuni ya simu za mkononi kwa jina la CELNET, baada ya kuingia kwa wawekezaji kampuni hiyo ilibadilishwa jina na kuitwa CELTEL ambayo iliwezeshwa na TTCL kimtaji, kiufundi, kimiundombinu na hesabu zake zilikuwa zikikaguliwa pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama