Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tanzania Yapaa Kiuchumi Afrika

Waziri wa Fedha na Mpango Mhe.Dr.Philip Mpango akiwaonyesha waandishi wa Habari mkoba wenye hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 leo Bungeni Mjini Dodoma tarehe 8th June 2018.

Na: Mwandishi Wetu

Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini imeendelea kuimarika ambapo Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/2018 bungeni leo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Tanzania inashika nafasi ya pili kwa ukuaji wa uchumi ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.1 nyuma ya Ivory Coast ambayo yenyewe uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.9.

Wabunge wakiingia Ukumbi wa Bunge kusikiliza hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 leo Bungeni Mjini Dodoma tarehe 8th June 2018.

Nchi zingine zilizokuwa na kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi ni Senegal (asilimia 6.6), Djibouti (asilimia 6.5) na Ethiopia (asilimia 6.5).

“Jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi”. Alieleza Waziri Mpango kwa kunukuu takwimu za Benki ya Dunia juu ya ukuaji wa uchumi nchini.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyoelezwa lakini bado kumekuwa na mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa hususan ukwasi katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini (private sector confidence)  na kwamba hali hiyo imesababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chefuchefu katika mabenki.

“Takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chefuchefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia 5.

Alifafanua kuwa Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016.

“Kupungua kwa kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania”. Alifafanua Dkt. Mpango.

Aidha katika bajeti hiyo, aliyataka mabenki yote nchini kusimamia kwa makini taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.

Alieleza kuwa ili kuimarisha ukwasi, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara  na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi.

Kwa mujibu wa Waziri Mpango, riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6 Machi 2017.

Aidha, ameeleza kuwa katika kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana (Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi na kwamba hatua hiyo imeanza kutumika rasmi mwezi Aprili 2017..

“Ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu”. Alieleza.

Katika eneo la mazingira ya kufanya biashara, Waziri mpango alieleza kuwa Serikali imeanza kuona viashiria bora zaidi katika eneo la kuboresha mazingira ya biashara.

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama