Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tanzania Yachaguliwa Mwenyekiti Baraza la Uongozi la AMGC

Na Jonas kamaleki

Tanzania imechaguliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC).

Uchaguzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 37 wa Baraza hilo uliofunguliwa jana na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wa Mkutano huo ambao ni mawaziri wa wanaohusika na sekta ya Madini wameipitisha Tanzania kwa kauli moja kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli wa kudhibiti na kusimamia raslimali Madini pia mabadiliko yanayofanywa kituoni hapo.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la AMGC, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe amesema Tanzania inathamini mchango wa Kituo hicho na kuongeza kuwa ndio maana Waziri Mkuu alifungua Mkutano wa Baraza.

Prof. Mdoe amewakumbusha nchi wanachama umuhimu wa kutumia Kituo hicho kwani kina vifaa vya kisasa vya kufanya uchunguzi wa maji na Madini ya kila aina.

Aidha, Prof. Mdoe ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa AMGC kutimiza wajibu wake muhimu katika kusimamia na kuendeleza Kituo hicho ambacho kina mchango mkubwa katika utafiti na uongezaji thamani ya madini.

“Wizara yangu itajitahidi kuhakikisha kuwa mpango kazi ambao tumeuidhinisha leo, unatekelezwa ipasavyo na kwa wakati kadiri tulivyokubaliana,”alisema Prof. Mdoe.

Akitilia mkazo maagizo ya Waziri Mkuu, Prof. Mdoe amesema kuwa yale ambayo yalisemwa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa yatekelezwe. Maeneo hayo ni pamoja na nchi wanachama kulipa ada na michango yao kwa wakati, AMGC kupewa ithibati ili kiweze kutoa huduma zake kwa viwango bora na vinavyokubalika kimataifa, nchi wanachama kutumia huduma za kituo kwa ukamilifu na kutangaza kazi na huduma za kituo ili kuvutia sekta binafsi kutumia huduma hizo.

Kwa kufanya hivyo kituo kitaimarika kifedha na kuacha utegemezi wa michango ya wanachama kujiendesha ikizingatiwa kuwa sasa kimepanda hadhi na kuwa cha Afrika nzima badala ya nchi nane wanachama wa sasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Lokeris Peter amesema kuwa Bara la Afrika linatakiwa kuvutia wawekezaji katika sekta ya Madini kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu.

Lokeris amesema kuwa Madini ni sekta ambayo inaweza kuziendeleza nchi za Kiafrika kiuchumi ikitumiwa na kusimamiwa vizuri.

“Tusisahau kuendeleza jamii inayozunguka maeneo ya migodi ya Madini, tuwafanye wajisikie kuwa sehemu ya wanufaika wa raslimali hizo muhimu zipatikanazo kwao,”alisema Lokeris.

Katika Mkutano huo Sudan imechaguliwa kuwa Makamu Mwenyeki huku Uganda ikichukua nafasi ya Ukatibu.

Mkutano huu umemalizika leo hadi mwakani utakapofanyika Sudan chini ya uenyekiti wa Tanzania.

 

67 thoughts on “Tanzania Yachaguliwa Mwenyekiti Baraza la Uongozi la AMGC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama