Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tanzania, Korea Zasaini Mkataba Ujenzi Daraja la Salander

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Lee Nak-yeon wakishuhudia tukio la utiaji saini Mkataba wa mradi wa ujenzi wa Ujenzi wa Daraja jipya la Selander litakalopita baharini kuanzia katika Hospitali ya Agha Khan hadi maeneo ya Coco beach jijini Dar es Salaam.

 

ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Lee Nak-yeon wakati wakielekea katika ukumbi wa Jakaya Kikwete uliopo Ikulu kwa ajili ya kushuhudia tukio la Utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja jipya la Selander litakalopita baharini kuanzia katika Hospitali ya Agha Khan mpaka Coco beach jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. Lee Nak-yon leo tarehe 23 Julai, 2018 wameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja la Selander linalounganisha eneo la hospitali ya Agha Khan na Coco Beach kupitia baharini Jijini Dar es Salaam, litakalojengwa kwa muda wa miezi 36 kuanzia sasa.

Mkataba wa ujenzi huo umetiwa saini na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Jee Hoon Kim kwa niaba ya Kampuni ya ukandarasi ya GS Engineering and Construction ya Korea.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali mara baada ya tukio la utiaji saini wa mradi wa ujenzi wa Ujenzi wa Daraja jipya la Selander litakalopita baharini kuanzia katika Hospitali ya Agha Khan mpaka Coco beach jijini Dar es Salaam.

Daraja hilo pamoja na njia zake litakuwa na urefu wa kilometa 6.23, likiwemo daraja lenyewe lenye urefu wa kilometa 1.030, litakuwa na njia 4 na litagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 250 za Tanzania hadi kukamilika kwake.

Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kutoa mkopo wa ujenzi wa daraja hilo, pamoja na miradi mingine ya maendeleo hapa nchini ikiwemo hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila na daraja la Kikwete lililopo katika mto Malagarasi mkoani Kigoma, na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Jamhuri ya Korea kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na wananchi wa Korea.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya Picha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Lee Nak-Yeon mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Mhe. Rais Magufuli ambaye kabla ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo amefanya mazungumzo na Mhe. Lee Nak-yon, amesema katika mazungumzo hayo ameiomba Korea kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ikiwemo utengenezaji wa meli kubwa katika ziwa Victoria ambayo mkataba wake utasainiwa hivi karibuni, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) katika vipande vitatu vilivyobaki na ujenzi wa daraja kubwa la urefu wa kilometa 3.5 litakalounganisha eneo la Kigongo na Busisi katika ziwa Victoria.

Kwa upande wake Mhe. Lee Nak-yon amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa imani aliyonayo kwa nchi ya Korea na amemuahidi kwenda kufanyia kazi maombi ya kushiriki katika ujenzi wa reli ya kati na daraja la Busisi-Kigongo.

Mhe. Lee Nak-yon amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Korea ina kampuni zenye ujuzi mzuri, uzoefu na teknolojia bora katika ujenzi na utengenezaji wa meli na kwamba anaamini kuwa kupitia ushirikiano mzuri wa Tanzania na Korea, wataalamu wa Tanzania watanufaika na pia Korea itaendelea kutoa nafasi za masomo kwa Watanzania kwenda kujifunza utaalamu mbalimbali nchini humo.

Aidha, Mhe. Lee Nak-yon amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na rushwa, kujenga miundombinu, kuhimiza watu kuchapa kazi na kuboresha huduma za kijamii, na amebainisha kuwa mafanikio makubwa ambayo yameiwezesha Korea kutoka katika kundi la nchi masikini miaka 60 iliyopita, hadi kuwa nchi yenye pato la mtu linalofikia dola za Marekani 30,000 kwa mwaka hivi sasa yametokana na hatua kama zinazochukuliwa na Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Lee Nak-yon amemaliza ziara yake ya siku 3 hapa nchini na kuelekea nchini Oman.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

23 Julai, 2018

One thought on “Tanzania, Korea Zasaini Mkataba Ujenzi Daraja la Salander

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama