Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taasisi za Fedha Zatakiwa Kuwawezesha Wajasiriamali

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha wageni katika banda la Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya J.K. Nyerere barabara ya Kilwa. (Na: Frank Shija)

Na: Frank   Mvungi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Taasisi za fedha kuwawezesha wajasiriamali ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumza  mara baada ya kutembelea maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Dar es Salaam (Sabasaba) Mama Samia  alisema kuwa taasisi za fedha zinaowajibu wa kuwawezesha wajasiriamali ili wapate mitaji ya kuendeleza biashara zao.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Samia Suluhu Hassan akitazama bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi katika moja ya banda alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya J.K. Nyerere barabara ya Kilwa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo,  Abdul Haleem Zahran kuhusu bidhaa za ujenzi zinazotengenezwa hapa nchini alipotembelea banda la Kampuni ya Property International katika Maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) leo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade Mhandisi Christopher Chiza.

“Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za fedha hapa nchini ili ziendelee kuwawezesha wajasiriamali na hatimaye kwa pamoja tufikie azma ya Tanzania ya Viwanda.”alisema Mama Samia.

Aidha Mhe. Samia alisema kuwa Maonesho ya mwaka huu yamezidi kuongeza ubunifu kutokana na kuongezeka kwa ubora wa bidhaa za ndani ya nchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Samia Suluhu Hassan akitazama samani zinazotengenezwa ndani ya nchi katika banda la Kampuni ya WOISO Product alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya J. K. Nyerere barabara ya Kilwa. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade Mhandisi Christopher Chiza na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage.

“Kwa ujumla niseme tu maonesho ni mazuri na tumeongeza muda ili watanzania wengi zaidi waje watembelee na kujionea bidhaa mbalimbali na huduma zinazotolewa “ Alisisitiza Mhe. Samia

Akifafanua amesema kuwa kuna mabadiliko makubwa hasa katika mabanda ya kina mama kwa kuwa bidhaa wanazozalisha zina ubora unaoendana na mahitaji ya soko.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji  Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa viwanda vyote walivyopewa wawekezaji vinaendelezwa na kuzalisha kwa tija.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda akifafanua jambo alipotembelea banda la Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (DITF) leo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Idara Kuu ya Biashara), Profesa Aldof Mkenda.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda akifuatilia maelezo kutoka kwa mmoja wa waonyeshaji katika eneo la bustani ya mahindi ya Kampuni ya uzalishaji wa mbegu ya Seed Co katika maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (DITF) leo.

Aliongeza kuwa Viwanda vya kuzalisha bidhaa za ngozi kama kile cha BORA sasa vimeanza uzalishaji kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali yaliyowataka wale wote waliopewa viwanda na Serikali kuviendeleza ili vitoe matokeo kusudiwa.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade Mhandisi Christopher Chiza ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ambapo kesho ni siku ya sikukuu ya sabasaba.

Maonesho haya ya Kimataifa ya 41 ya Biashara Dar es Salaam (DITF) yalianza Juni 28 na yanatarajiwa kumalizika Julai 13 ambapo yanashirikisha takribani nchi 30 na Makampuni zaidi ya 2500 huku kauli mbiu yake ikiwa ni “Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda”.

68 thoughts on “Taasisi za Fedha Zatakiwa Kuwawezesha Wajasiriamali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama