Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

 

DENI LA TAIFA HALIJAONGEZEKA KWA SH. TRILIONI 12

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshitushwa na taarifa potofu zilizochapishwa na gazeti la Mwananchi toleo Na. 6499 la tarehe 17 Mei 2018 kuhusu Deni la Taifa na kusema taarifa hizo sio sahihi na zinapaswa kupuuzwa. Katika toleo hilo, gazeti hilo lilidai kwamba kulikuwa na ongezeko la sh. trilioni 12 katika deni la taifa kati ya Desemba 2017 na Machi 2018, takwimu ambazo sio sahihi.

 Takwimu sahihi ni kwamba Deni la Serikali pekee liliongezeka kwa sh. trilioni 2 kutoka sh. trilioni 47 hadi sh. trilioni 49. Deni hilo linajumuisha mikopo kutoka nchi wahisani, mashirika ya fedha ya kimataifa pamoja na mabenki ya kibiashara ya kimataifa wakati deni la ndani la Serikali linajumuisha dhamana za Serikali za muda mfupi na hati fungani za Serikali pamoja na madeni mengineyo.

Aidha, Deni la nje la sekta binafsi kati ya mwezi Desemba 2017 na Machi 2018 liliongezeka kwa sh. trilioni 1.0 tu, kutoka sh. trilioni 9 hadi sh. trilioni 10. Hivyo, Deni la Taifa, ambalo linajumuisha Deni la Serikali la ndani na nje na deni la nje la sekta binafsi, liliongezeka kwa sh. trilioni 3 kutoka sh. trilioni 56 mwezi Desemba 2017 hadi sh. trilioni 59 mwezi Machi 2018.

Ongezeko la Deni la Taifa linatokana na mikopo mipya kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na malimbikizo ya riba, hasa kutoka nchi za kundi lisilo la wanachama wa Paris, ambazo hazijatoa misamaha ya madeni kulingana na makubaliano.  Pamoja na ongezeko hilo, Deni la Taifa bado ni himilivu. Aidha, kuongezeka kwa Deni la Taifa kunatokana na jitihada za Serikali kujenga mazingira bora zaidi ya kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Badala ya kulinganisha takwimu zinazofanana, gazeti la Mwananchi limelinganisha takwimu za Deni la Serikali la Desemba 2017 na Deni la Taifa la Machi, 2018 ambazo zinajumuisha vitu tofauti. 

Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania inalitaka gazeti hilo kuchapisha taarifa ya takwimu sahihi kwa uzito ule ule kama lilivyopotosha. Aidha, tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuomba ufafanuzi wa masuala yanayohusu taasisi hii ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza kwa kuchapisha taarifa zisizo sahihi.

BENKI KUU YA TANZANIA

Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki

botcommunications@bot.go.tz

19 Mei 2018

376 thoughts on “Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama