Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Wagonjwa 16 Wenye Matatizo Ya Moyo Wafanyiwa Upasuaji Wa Kufungua Kifua

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International (OHI) ya nchini Australia tumefanya upasuaji  wa  kufungua kifua kwa wagonjwa  16 wenye matatizo ya Moyo. Kati ya hao watoto ni tisa  na watu wazima saba .

Upasuaji huu umefanyika katika kambi maalum ya matibabu ya Moyo iliyoanza tarehe 25/11/2017 na kumalizika leo  tarehe 01/12/2017.

Wagonjwa watu wazima tumewafanyia upasuaji  wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting) na kubadilisha milango ya moyo miwili hadi mitatu iliyokuwa imeziba au haifungi vizuri.

Kwa upande wa watoto tumefanya upasuaji na vipimo kwa watoto ambao vyumba vyao vya moyo havijakamilika na hivyo damu kwenda kwa wingi kwenye mapafu. Kuwafanyia watoto vipimo tukiwa tumefungua vifua inasaidia kufahamu aina ya upasuaji  tunaotakiwa kuufanya.

Upasuaji tuliowafanyia watoto ni wa awali  ili kuutayarisha moyo kwa ajili ya upasuaji mwingine ujao. Watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi hii ni wenye uzito wa kuanzia kilo nne hadi 12 ambao  umri wao ni miezi minne hadi miaka minne.

Kwa mara ya kwanza tumeweza kufanya upasuaji kwa mtoto ambaye moyo wake ulikuwa upande wa kulia  na vyumba vyote vya moyo vinafanana wakati vinatakiwa kuwa tofauti . Katika upasuaji huu tumeweza kulinda mapafu yalikuwa yanapokea  damu kwa wingi kutoka kwenye mishipa ya moyo. Mtoto huyu pia tumeweza kumuwekea kifaa ambacho kitamsaidia moyo wake kufanya kazi vizuri (Pace Maker).

 Kwa namna ya kipekee tunawashukuru sana wenzetu hawa wa OHI kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na sisi kutoa matibabu  kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo. Pia wamekuwa wakitoa mafunzo kwetu ambayo yametusaidia sana kuongeza ufanisi wa kazi. Kabla ya kuanza kambi hii kulikuwa na mafunzo kwa wauguzi wetu ambao walifundishwa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa waliopo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).

Aidha tunawaomba wananchi waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu  wakati wanapatiwa  matibabu. Kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wanaopenda  kuchangia damu tunawaomba  wafike Taasisi ya Moyo iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa maelezo zaidi wawasiliane kwa simu namba 022-2151379 au 0713304149.

Naomba nimalizie kwa kuwahimiza wananchi ambao bado hawajajiunga na mifuko ya bima ya afya waweze kujiunga kwani matibabu hasa ya moyo gharama zake ni kubwa. Kujiunga na mifuko ya bima ya afya kutawasaidia kulipia gharama za matibabu pindi  watakapougua.

 Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Imetolewa na:

Kitengo cha Uhusiano na Masoko

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

01/12/2017

 

29 thoughts on “Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama