Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekemea tabia iliojengeka nchini ya wanamichezo ku[peleka kesi za michezo mahakamani, na kusema hatua hiyo imekuwa ikidumaza maendeleo ya michezo nchini  .

Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Uwanja wa Mao Tse Tung uliopo Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharibi ambao umejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mashirikiano ya pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema  michezo ni jambo la ridhaa na maelewano, hivyo matatizo yote yanayojitokeza, ni lazima yashughulikiwe na kumalizwa kwa busara.

Alitoa indhari kwa kubainisha kuwa kuanzia sasa hatokuwa tayari kusadia shughuli za kimichezo, ikiwemo soka  endapo tabia ya kupeleka kesi hizo mahakamani itaendelea.

“Acheni tabia hiyo mnaitia aibu nchi yetu, nataka nikwambieni kuwa FIFA inatuonea imani tu juu ya jambo hilo, ni matumaini yangu kuwa kesi za michezo hazitafikishwa tena mahakamani” alisema.

Aidha, Dk. Shein alisema Serikali inakusudia kuongeza bajeti ya Wizara ya Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo  kuanzia mwaka ujao wa fedha, ili kuimarisha na kuendeleeza michezo mbali mbali nchini.

Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu, ili kuleta ushindani na kuwa miongoni mwa timu bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itahakikisha inafanikisha azma yake ya kujenga Uwanja mkubwa wa kisasa utakaochukua watu 45,000 kutoka maeneo yaliyotengwa huko Fumba pamoja na Tunguu.

Katika hatua nyengine  Dk. Shein aliigiza Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na michezo kuandaa programu nzuri itakayowezesha matumizi bora ya kiwanja hicho, ili uweze kudumu.

Alisema ni vyema kukawepo  utaratibu wa kuweka viingilio katika baadhi ya mashindano ili kuweza kupata fedha zitakazowezesha kukifanyia matengenzo madogo madogo kiwanja hicho pale panapohitajika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ujenzi wa uwanja huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Nae Waziri wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Balozi Ali Abeid Karume alitoa shukurani na pongezi kubwa kwa Rais Dk. Shein kwa jitihada zake za kuhakikisha uwanja huo unajengwa upya na una kuwa wa kisasa.

Balozi  Karume alimponmgeza Dk. Shein kwa kuweka kipaumbele suala la kuimarisha michezo, hivyo, akaahidi Wizara yake kuwaendeleza vijana pamoja na kukitunza ipasavyo kiwanja hicho.

Aidha, Balozi Karume alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na matunda ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Nae Balozi Mdogo wa China anaefanya kazi zake hapa Zanzibar Xie Xiuowu alisema ujio wa mradi huo utaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar.

Aidha, alisema kukamilika kwa kiwanja hicho pamoja na ujenzi wa viwanja mbali mbali vya michezo ya ndani (indoor games) kutaimarisha viwango vya wanamichezo wa Zanzibar na hivyo kufanya vyema katika mashindano mbali mbali ya .

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Omar Hassan (King) alieleza kuwa jumla ya gharama zote za mradi zilikuwa ni TZS Bilioni 15 ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China walitoa msaada wa TZS Bilioni 11.

Alisema kuwa mradi huo ulikuwa na maeneo ambayo yaligharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na maeneo mengine yaligharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo mpaka sasa fedha zote zimelipwa na hakuna deni lolote linalodaiwa.

Aliongeza kuwa mradi huo ulianza rasmi tarehe 3 Machi 2017 na ulitakiwa ukamilike mwishoni wa mwezi wa Mei, 2018 kwa kazi zile zilizomo kwenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Alieleza kuwa hata hivyo, baada ya kuangalia kwa makini ikaonekana kwamba kuna haja kubwa ya kumalizia maeneo yote ya uwanja ili uwanja upendeze zaidi hasa maeneo ya ukuta pembezoni mwa uwanja kwa kujaza zege nyengine.

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa kupitia mahitaji hayo, ndipo kukapelekea kuchelewa kwa ujenzi huo kwa muda wa miezi mitatu na hadi ilipofika mwezi Agosti, 2018 ambapo kwa msaada wa Serikali ya China zilikuwa zimekamilika na kufikia Novemba 2018 kazi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nazo zilikamilika.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo katika mkataba huo wa ujenzi wa “Zehngtai Group Company” baadhi yao watabaki hapa Zanzibar kwa muda wa miaka miwili ili kuangalia kama kutakuwa na matatizo yoyote makubwa ili yafanyiwe marekebisho.

Katibu Mkuu huyo aliyataja maeneo ambayo yametekelezwa kupitia fedha za msaaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo ni uwanja wenyewe ambao una viwanja viwili vya mchezo wa mpira wa miguu ambayo vina vipimo vya Kimataifa na vimewekewa nyasi bandia.

Mengine ni majukwaa mawili makubwa na mawili madogo yenye uwezo wa kuchukua watazamaji 2,100, uwanja wa kucheza aina nne za michezo ikiwemo “Bastektball” na “Volleyball” ambapo pia, kuna sehemu ya michezo ya ndani (Indoor) ikiwemo kucheza “Table Tennis” ambayo ina jumla ya meza sita.

Mambo mengine yaliyotekelezwa ni kuwepo kwa sehemu ya mazoezi ya viungo ya kuinua vitu vizito (Gym nastic), jengo la vyoo 48 kwa ajili ya huduma za jamii, majengo mawili kwa ajili ya Ofisi na ujenzi wa ukuta kwenye eneo la Mashariki.

Akiyataja mambo ambayo yametekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu huyo aliyataja kuwa ni pamoja na kusafisha eneo lote la uwanja wa Mao kwa kubomoa majengo ya zamani, kuwapatia eneo wakandarasi kwa ajili ya kuweka makaazi yao, kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana zikiwemo maji na umeme.

Mambo mengine ni kugharamia huduma za ulinzi kwa muda wote katika eneo la kiwanja, kulipa gharama zote za utoaji wa vifaa bandarini na wuanja wa ndege, kujenga ukuta wenye urefu wa mita 220 upande wa Magharibi, kujenga kwa kujaza zege eneo lote la pembezoni mwa uwanja pamoja na kuweka mfumo wa kutoa maji kwenye uwanja kwa kuchimba chini mashimo 36 ambayo hupeleka maji kwenda chini.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na mamia ya wananchi walihudhuria katika sherehe hiyo ya uzinduzi wa uwanja huo ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

20 thoughts on “Taarifa kwa Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama