Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

RC Makonda Aunga Mkono Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul makonda amepongeza jitihada za Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi (TACIP) ambao unalenga kuwarasimisha wasanii nchini ili waweze kunufaika na kazi zao.

Makonda amesema hayo ofisini kwake jijini Ilala, jijini Dar es salaam wakati alipotembelewa na wajumbe wa TACIP ili kumtambulisha kuhusu mradi huo ikiwemo malengo yake na utekelezaji wake katika mkoa wa Dar es Salaam.

Wajumbe wa mradi huo waliofika kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mungereza, Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamalle, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara na Mahusiano wa DataVision International, Teddy Qirtu na Ofisa wa mradi wa TACIP katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mfaume pamoja na wengine.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mungereza akitambulisha ujumbe huo wa TACIP kwa Mh. Paul Makonda alisema kuwa mradi huo ambao upo chini ya Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo inayoongozwa wa Waziri wake Dkt. Harrison Mwakyembe unalenga kuwafikia wasanii wote wa Sanaa za Ufundi nchini, ili kuwatambua na kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbali mbali katika kazi zao.

Amesema kuwa wasanii wa kazi za ufundi wamekuwa katika mazingira magumu ya kazi zao na kushindwa kupenya kwenye hadhi ya kimataifa kwa sababu mbalimbali moja ikiwa ni fani hiyo kutokuwa na umoja ambao unaweza kuwakutanisha pamoja na kupanga jinsi ya kupanua soko la bidhaa zao, hivyo TACIP itawewezesha kujitanua kiuchumi kuliko wanavyoonekana katika sura ya umaskini kwa sasa.

Naye Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamale amemweleza Mh. Makonda namna mradi huo utakavyofanya kazi, amesema kuwa kwa kutambua changamoto za wasanii hao, TACIP inaenda kuzitatua kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwasajili wasanii hao, kuwapa vitambulisho ambavyo vitawatambulisha popote watakapokuwa wanafanya kazi zao za sanaa, pia kupitia vitambulisho hivyo wataweza kukopesheka katika mabenki na kuongeza mitaji yao.

Mbali na faida hizo, TACIP inaenda kuongeza thamani ya msanii aliyejiunga na mradi huo, kwani hatahitaji dalali wa kuuza kazi zake bali yeye mwenyewe ataweza kuonekana na kuuza kazi zake kupitia teknolojia kubwa iliyotengenezwa na Kampuni ya DataVision International ambayo imebobea katika masuala hayo.

Nyangamale amesema wasanii wanakutana na ugumu kwasababu kazi za ufundi kutozungumza kama ulivyo muziki au filamu ambazo ni rahisi kwa mtu kujua ni nani aliyeigiza au kuimba.

“Sanaa yetu ina changamoto kubwa na kati ya changamoto zenyewe ni hizi kazi zetu kutokuimba kama wasanii wanaoimba au kuigiza ambako ni rahisi watu kujua aliyeimba au aliyeigiza ni nani.

“Ni wazi unaweza kupata jibu kwenye hili ninalosema katika mfano wa karibuni zaidi pale watu kadhaa walipojitokeza kudai ni wachoraji/wachongaji wa Nembo ya Taifa. Kama kinyago kile kingekuwa kinaimba au kuigiza, ingekuwa rahisi kujua ni nani aliyeimba, maana tungesikia sauti ya mwimbaji.”

Nyangamale amesema kupitia TACIP kwa sasa hali hiyo inakwenda kubadilika kwa vile wameingia katika makubaliano maalumu na DataVision International ambayo itachukua jukumu la kutafiti idadi halisi na kuwatambua wasanii wa sanaa za mikono nchini na kupanga jinsi ya kuwasaidia kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia.

“Tunaamini kupitia teknolojia ya DataVision katika mradi huu wasanii wataweza kupata thamani ya jasho lao wanalovuja juu ya kazi hizi, na tutawafikie wasanii wote wa ndani ya Dar es Salaam na nje kwa urahisi, kuliko tukiendelea kukaa katika hali tuliyokaa huko nyuma.”

Nyangamale ameongeza kwamba sanaa ya uchongaji haiko Dar es Salaam pekee, bali iko nchi nzima, hivyo ushirikiano wao na DataVision International kuwatambua wasanii wote kwa majina, makazi na kazi zao ambazo zote zitaweza kuonekana kwenye tovuti (Web Portal) ambayo itakuwa mahsusi kwa sanaa tu, hivyo kuwezesha watu na asasi mbalimbali duniani kote kujua uwezo wa wasanii wetu.

Amesema hadi sasa tayari wameshaanza majaribio na yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wasanii wameanza kutambulika, kushiriki katika matamasha na wengine kuanza kupokea mikopo kwa urahisi kabisa kupitia mradi huo wa TACIP.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara na Mahusiano, Teddy Qirtu amesema kuwa Kampuni ya DataVision International ambayo inatimiza miaka 20 sasa inauzoefu mkubwa katika masuala ya teknolojia na imekuwa ikifanya ubunifu wa mifumo mbali mbali Serikalini na katika Taasisi na Mashirika binafsi ndani na nje ya chi, hivyo kupitia uzoefu huo wamebuni mfumo huo wa TACIP ambao unaenda kuwasaidia wasanii wa sanaa za ufundi.

Amesema wametengeneza ‘Web Portal’ ya wasanii wote nchini kisha kuwawezesha na kuwaelimisha juu ya nguvu ya teknolojia katika kupenya kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi ili waweze kusonga mbele.

Pia ameeleza kuwa kuna vitambulisho vya TACIP ambavyo vinauwezo wa kuhifadhi taarifa za kila msanii ambaye amesajiliwa, pia msanii ataweza kuuza na kuvusha bidhaa zake kwa urahisi bila usumbufu wowote awapo na kitambulisho hicho.

Baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa Ujumbe wa TACIP, Makonda ameeleza furaha yake kwa mradi huo na kuupokea kwa mikono miwili ambapo amewapongeza watendaji wote wa mradi huo.

“Nawapongeza sana, mradi huu unakuja na mabadiliko yakipekee katika sanaa yetu nchini, nawakaribisha na nitasiamama pamoja nayi kuhakikisha mradi huu unatimiza malengo yake kwa lengo la kuisaidia Serikali lakini pia kuwaletea maendeleo vijana wetu na watanzania kwa ujumla” Amesema Makonda.

Aidha, Makonda ameishukuru Kampuni ya DataVision International kwa kuweza kubuni mfumo ambao sasa unaenda kuwa msaada kubwa kwa wasanii  nchini.

 

49 thoughts on “Taarifa kwa Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama