Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TAA Yatakiwa Kuhakikisha Viwanja Vilivyoboresha Vinaacha Kuitegemea JNIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiwasili na ndege aina ya Bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), mkoani Tabora katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo jana.

Na:  Tiganya Vincent. RS –Tabora

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA) imetakiwa kuhakikisha kuwa viwanja vya ndege vilivyoboreshwa vinajisimamia na kujiendesha vyenyewe ili viache kutegemea mapato kutoka Kiwanja cha Kimatifa ya Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbawara jana mjini Tabora mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa Ndege wa Tabora,

Alisema kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege mbalimbali na ununuzi wa ndege mpya kiasi cha kuwepo hapa nchini.

Profesa Mbawara alisema kuwa viwanja vilivyopo kabla ya maboresha  vilikuwa na mapato kidogo sana na kutegemea mapato kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Waziri huyo wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano alisema kuwa kutokana na uboreshaji uliofanyika na mwelekeo mzuri wa upatikanaji wa abiria kuanza kuwa mzuri , hakuna sababu ya kuendelea kutegemea fedha za uendeshaji kutoka JNIA  ni vema waanze kujitegemea kwa kutumia mapato wanayokusanya.

“Ukiangalia mwelekeo wa abiria unavyobadilika mwaka jana Tabora kuliwa na abiria elfu 16…mwaka huu nafikiria abiria wanaweza kufika elfu 26 mwakani na  kufika elfu 30…viwanja hivi lazima sasa vianze kujisimamia na kujiendesha vyenye bila kutegemea uwanja wa Dar es salaam” alisisitiza Profesa Mbawara.

Alisema kuwa kinachotakiwa kwa Watendaji wa Viwanja vilivyoboreshwa ni uadilifu na matumizi mazuri ya mapato ili viweze kuimarika zaidi na kutoa huduma nzuri kwa watumiaji wa viwanja hivyo.

Aidha Profesa Mbawara aliwaomba wananchi hasa  wakazi wa Tabora ambapo Uwanja umeboreshwa kuhakikisha wanalinda miundo mbinu yake ambao imegharimu shilingi bilioni 27 ikiwa ni mkopo toka Benki ya Dunia ili uweze kudumu kwa muda mrefu na uwe salama kwa usafiri huo.

Kwa upande  wake Meneja Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Tabora Mhandisi Neema Joseph alisema ukarabati wa Uwanja huo ulihusisha uwekaji wa lami katika njia ya pili ya ndege kuondoka na kutua  ambayo pia inatumika kwa ndege kwenda kwenye maegesho.

Alisema kuwa ukarabati mwingine ulikuwa  na kuweka taa za kuongozea ndege na mitambo wa kisasa wa kuongoza ndege hata kama iko mbali mrefu.

Mhandisi Neema aliongeza kuwa ukarabati wa Uwanja huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha wiki mbili zijazo kwa kuwa umefikia asilimia 95 na mara baada ya kukamilika Uwanja wa Tabora utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa na ndogo katika saa 24 kwa siku na kipindi chote cha mwaka.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya EMF Aviation Services Limited Ernest Mgongolwa alisema mtambo kuongozea ndege unafungwa katika Uwanja wa Tabora ni miongoni mwa mitambo ya kisasa na una uwezo wa kuongoza ndege zinapita hata umbali wa Kilometa 200.

Alisema kuwa mitambo ya aina hii ipo katika Uwanja JNIA, Kilimanjaro, Zanzibar, Mwanza na sasa unajengwa Tabora.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama