Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

SUMA JKT Yaendelea Kutekeleza Dhima ya Tanzania ya Viwanda

Na:  Immaculate Makilika

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT),  linatarajia kuanzisha kiwanda cha kusindika minofu ya nyama ya ng’ombe na samaki  na kampuni ya kusambaza nyama kwa nia ya kuunga mkono azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa kwa ushirikiano kati ya  Idara ya Habari, (MAELEZO) na kurushwa na kituo cha televisheni cha TBC1,  Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT  Brigedia Jenerali  Charo Yateri alisema kuwa shirika hilo pia   limedhamiria kutoa  mafunzo kwa vijana kupitia miradi mbalimbali ambayo ipo chini ya shirika hilo.

 “SUMA JKT imeendelea kujiimarisha kupitia miradi yake ya   kilimo, huduma za ulinzi, uvuvi pamoja na ufugaji, ambapo ina viwanda vya kusindika na kuchakata mazao, na asali ambapo kupitia miradi na viwanda hivyo imetoa  ajira 4,500 kwa vijana nchini” alisema Brigedia Jenerali Yateri.

Alitaja viwanda hivyo kuwa ni viwanda vya kusindika asali mkoani Tabora, viwanda vya kusindika na kuchakata nafaka vilivyopo Mlale mkoani Ruvuma  na Mafinga mkoani Njombe.

Mbali na hayo, Brigedia Jenerali Yateri alisema kuwa SUMA JKT ina miradi mbalimbali ikiwemo ya kujenga majengo  ya Halmashauri, barabara kwa  gharama  nafuu, ubora na uharaka Nna wana mpango wa  kujenga nyumba za wanajeshi kwa ajili ya kuwakopesha.

“ Tunaendelea kufanya mazungumzo na benk ya Azania  ili tujenge nyumba za wanajeshi ambapo wataweza kupewa mikopo ya kununua nyumba hizo, na baadae tutaanza kujenga nyumba kwa wananchi” alisema Brigedia Jenerali Yateri.

Alitaja  huduma nyingine zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni pamoja na  kuuza zana bora za kilimo kama matrekta, pampu za maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kufundisha jamii kilimo, uzalishaji wa mbegu bora za nafaka na mradi wa  mabwawa ya kufuga samaki katika vizimba vya  ziwa Victoria

Aidha, Brigedia Jenerali Yateri alisema SUMA JKT inajivunia  miradi hiyo  sambamba na kuwa na kilimo cha mazao ya  biashara kama vile kahawa mkoani  Mbeya na mchikichi mkoani Kigoma, sambasamba na uwezo wa  kujitegemea kwa asilimia 55, huku ikipata ruzuku ya serikali asilimia 45 tu.

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), lilianzishwa mwaka 1982, kwa tamko la Rais chini ya sheria ya uanzishaji wa mashirika ya ummakwa lengo la kuisaidia  serikali kupunguza gharama za kuendesha mafunzo kwa vijana wanaopatiwa ujuzi wa aina mbalimbali ili kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na  Taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama