Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

SUA Kuokoa Asilimia 40 ya Mazao Yanayoharibiwa na Panya Shambani

Na: Judith Mhina – MAELEZO

Mojawapo ya sababu zinazowakosesha Wakulima kupata mazao mengi shambani ni viumbe hai waharibifu ambao hushambulia mbegu au mazao yenyewe kabla na baada ya kuvunwa.

Kutokana na hali hii uzalishaji wa mazao shambani unapungua na pia kiasi kidogo kinachopatikana baada ya kuvuna nacho hupungua kutokana na viumbe hao waharibifu kuendelea kuharibu kikiwa ghalani. Aidha, hali hii kuwakosesha Wakulima kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa mtafiti kutoka Kituo cha Viumbe Hai Waharibifu wa Mazao na  Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine – SUA, Dkt. Christopher Sabuni, aliyenukuliwa kupitia kipindi cha “Ukulima Bora” kinachorushwa na TBC FM, viumbe hai waaribifu wa mazao wapo wengi na wamegawanyika katika makundi tofauti kama vile wanyama, wadudu, na ndege.

Amewataja viumbe hai waharibifu katika mazao ya kilimo wanaotambulika sana na wakulima hapa nchini ni pamoja na  panya, kupe, dumuzi, mdudu Cytophilus au tembo, viroboto, kupe, mmbu na wengineo.

Amesema, jukumu la Kituo cha Viumbe Hai Waharibifu wa Mazao ni pamoja na kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kuokoa mazao ya wakulima yasiharibiwe na wadudu ili kumwezesha mkulima kupata mazao mengi zaidi.

Kutokana na jukumu hilo, Kituo hicho kimefanya utafili wa kudhibiti panya waharibifu wa mazao ambapo kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo asilimia 40 ya mazao mashambani yataokolewa. Dkt. Sabuni amesema utafiti huu una manufaa mengi kwa mkulima ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ufundishaji na udhibiti wa uharibifu wa mazao.

“Hata hivyo, tunalenga kutoa elimu kwa mkulima ni kwa jinsi gani anaweza kupunguza hasara ili aweze kufaidika na nguvu zake kwa kuvuna chakula kingi iwezekanavyo,”amesema

Akifafanua zaidi kuhusu wanyama waharibifu amesema, kuna aina 2276 za panya ambao hupatikana karibu sehemu nyingi duniani. Hawa ni wanyama ambao hunyonyesha isipokuwa aina chache sana ambao hazipatikani maeneo mengine. Panya wenye kutia hasara ni wale  wanaokula nafaka, matunda na mazao aina ya mizizi kama mihogo, viazi nk.

Panya wenye kutia hasara kubwa barani Afrika hususani kusini mwa Jangwa la Sahara ni wale wanaokula nafaka, viazi na pamba. Panya hawa hujulikana kwa jina la  Shambarat au mutmanitret.  Aidha, panya hawa wana matiti mengi na ustawi sana mashambani na kwenye mapori. Wana uwezo wa kuzaa watoto 20 kwa wakati mmmoja na huongezeka kwa wingi.

Kutokana na wingi wao wanao uwezo wa kula mbegu zikiwa shambani wakati wa kupanda maana zinatoa harufu na kuwa kichocheo kinachowafanya kufuatilia na pia zinapokuwa zimehifadhifa ghalani.

Aina nyingine ya panya ni wale wanaoishi majumbani katika paa la nyumba ambao hujulikana kwa jina la Roofrat. Aina nyingine ya panya wa ndani ni Ratus ratus wanaoishi ghalani lakini pia huweza kutoka nje na kula lakini mara nyingi hukaa ndani.

Fuko ni aina nyingine ya panya anayeshinda kwenye mashimo na kula mazao ya mizizi kama vile mihogo, viazi na mizizi mingine ya porini. Panya huyu ambaye haoni anatumia sana kunusa kuweza kutambua chakula. Akitoka nje ya shimo inakuwa vigumu kutembea kutokana kuwa katika mazingira mageni. Fuko anatofautiana na panya wengine kwani ni mkubwa kwa umbo.

Aina nyingine ya panya ni wale wenye rangi mweupe ambao mara nyingi wanatumiwa katika maabara. Panya hawa ambao ni wadogo ukilinganisha na wengine wanakosa rangi ya asili huzalishwa kwa wingi kwa ajili ya kutumika katika tafiti mbalimbali.

Panya wengi wanatofautiana kwa maumbile na maeneo wanayoishi. Panya mkubwa zaidi ana uzito wa kilo 25 na hupatikana nchini Australia, mdogo ana gram 4.

Udhibiti  wa panya

Kwa mujibu wa Dkt Christopher Sabuni, kuna aina mbalimbali za kuweza kudhibiti panya waharibifu. Njia ya kwanza ni kuhakikisha kwamba shamba linakuwa safi. Fanya usafi mita 10 kutoka katika shamba lako ili panya wakose eneo la kujificha kutoka katika mpaka wa shamba. Kutokana na usafi huu shamba lako linakuwa vigumu kuvamiwa na panya kwa sababu watakosa sehemu ya kujificha, kuzaliana  na kutengeneza makao.

Pili, kutumia viatilifu ambavyo vinanyunyuziwa kwenye mashamba.  Hata hivyo utafiti unaendelea kuweza kupata viatilifu vitakavyolenga kuangamiza panya tu. Kwa sasa viatilifu vilivyopo vinaua hata wale wasio waharibifu. Vile vile, utafiti huo unalenga kupata viatilifu ambavyo havitakuwa na madhara kwa binadamu.

Tatu, utafiti huo umegundua matumizi ya vidonge vya uzazi kwa panya waaribifu wa mazao. Vidonge hivyo vyenye harufu ya kuwavutia huwekwa katika maeneo ambayo yataonekana kuwa ni makazi yao na hivyo watakapokula watakuwa wamepunguzwa uwezo wa kuzaana.

Nne, matumizi ya mifuko sahihi isiyopitisha hewa na kufanya mazao kuwa salama unapohifadhi nafaka iitwayo Hemetic Bags. Mifuko hiyo imetengenezwa bila kutumia dawa ya aina yeyote. Unapoweka nafaka ndani ya mfuko na kuufunga bila ya kupitisha hewa, harufu ya nafaka haitoki na hivyo panya wanashindwa kujua kama kuna nafaka ndani yake na kushambulia mfuko.

Mifuko hiyo ambayo inatengenezwa mkoani Tanga imeanza kutumiwa na wakulima wa mikoa ya Njombe, Morogoro, Mbeya na Iringa. Aidha,  wajasiriamali wanaagiza mifuko hiyo kupitia Halmashauri zao kulingana na mahitaji yao.

Tano, udhibiti wa panya hufanywa kwa kutumia mtego aina ya Treebit Beilar System – TBS. Mtego huu unaotoa harufu inayowavutia huwekwa katika eneo dogo la shamba lililopandwa mazao kama sehemu ya kuwatega na kuwakamata (catching point). Unapoona idadi ya panya imepungua sasa unaweza kupanda shamba zima uliloliandaa.

Kwa mujibu wa utafiti wa Kituo cha Viumbe Hai Waharibifu wa Mazao, pia wapo panya ambao wanakula majani tu. Panya hao  ni waharibifu kwenye bustani za makazi ya watu au bustani. Mkulima anayezingatia na kutumia mbinu zilizoelezewa na Kituo hiki, atafaidika katika kuokoa asilimia 40 ya mazao yake ambayo yangepotea na kujiongezea kipato cha familia yake na Taifa kwa ujumla.

 

50 thoughts on “SUA Kuokoa Asilimia 40 ya Mazao Yanayoharibiwa na Panya Shambani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama