Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Yazigeukia Kampuni Zinazotandaza Nyaya z Umeme Kwenye Majengo

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), akimkabidhi pesa ya kulipia gharama za kuunganishiwa umeme mzee mwenye umri wa miaka 109, Ramadhan Manga, mkazi wa kijiji cha Muungano, Morogoro Vijijini kutokana na uzalendo aliouonesha, kuruhusu mazao yake yakatwe kupisha njia ya umeme, pasipo kudai fidia. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi, Agosti 28, 2019.

Na Veronica Simba – Morogoro

Serikali imetoa rai kwa kampuni zinazotandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo maarufu kama ‘wiring’ kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama zao hususan kwa wananchi walioko vijijini ili waweze kuzimudu.

Rai hiyo ilitolewa Agosti 28 mwaka huu na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), akimhamasisha mkazi wa Msonge, Morogoro Vijijini, kuutumia umeme aliounganishiwa kuboresha biashara yake ya kuchakata mafuta ya mawese, kwa kununua mashine ndogo badala ya kutumia mkono, ili kuboresha kipato chake. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi, Agosti 28, 2019.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (mbele), akiwa amefuatana na ujumbe wake wa viongozi na wataalamu wa serikali, kwenda kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Muungano, Morogoro Vijijini (hawapo pichani), akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 28, 2019.

Alisema kampuni hizo zinatakiwa kutambua kuwa serikali imezitengenezea fursa kutokana na kupeleka miundombinu ya umeme maeneo ya vijijini, la sivyo wasingepata wateja hivyo nazo zinawajibika kuangalia hali za wananchi hao kwa kuiga mfano wa serikali ambayo imewapunguzia gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 177,000 hadi kufikia 27,000 tu.

“Hizi bei za laki mbili hadi tatu, kwakweli siyo rafiki kwa wananchi wengi wa vijijini ambao serikali imewapunguzia gharama za kuunganishiwa umeme kutokana na uwezo wao. Sasa hawa wenzetu watafakari, itafika mahala umeme utafika, wananchi wanaounganishwa ni wachache na wao watakosa biashara.

Naibu Waziri aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia namna ya kusaidia jambo hilo. “Hatuna nia ya kuwadhibiti moja kwa moja, lakini waangalie ili bei ziendane na hali za watanzania vijijini pamoja na malengo ya kiserikali,” alifafanua.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa pili-kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya State Grid Electrical & Technical Works Ltd, WinGod Siyao (wa pili-kulia), anayetekeleza mradi wa umeme Morogoro Vijijini kuhusu hatua iliyofikiwa katika kazi hiyo. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi eneo la Tununguo, wilayani humo, Agosti 28, 2019.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikati), na ujumbe wake, wakikagua miundombinu ya umeme katika kijiji cha Tambuu, Wilaya ya Morogoro Vijijini, alipokuwa katika ziara ya kazi, Agosti 28, 2019.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuongeza kasi na kusema kuwa serikali haitawaongezea muda bali itaendelea kusimamia makubaliano baina yao, kwamba ifikapo Desemba mwaka huu, wawe wamekamilisha ujenzi wa miundombinu husika na kubaki kazi za kuwaunganisha wateja.

Aidha, alitoa rai kwa wananchi vijijini ambao wameshafikiwa na miundombinu ya umeme wachangamkie fursa kwa kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishwe na kuutumia umeme kujiletea maendeleo.

“Wakati mwingine inatunyong’onyesha tunapokuta baadhi ya maeneo watu wana uhitaji mkubwa wa umeme lakini miundombinu haijawafikia na sehemu nyingine mradi umefika, watumiaji wachache.”

Wananchi wa Kijiji cha Tambuu, Morogoro Vijijini, wakitawanyika, baada ya kushuhudia tukio la Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (hayupo pichani), kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, Agosti 28, 2019.

Vilevile, Naibu Waziri aliwasisitiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ngazi ya wilaya na mikoa, kuendelea kutekeleza agizo la serikali la kuwaunganishia umeme wananchi wa vijijini kwa bei ya shilingi 27,000 tu pasipo kuwalipisha nguzo na vifaa vingine.

Pia, alitoa onyo kwa mameneja kuacha kuwajibu wananchi wanaopeleka maombi ya kuunganishiwa umeme kwa gharama iliyoainishwa na serikali, kuwa bado hawajapata waraka husika. Alisema, Waraka wameshaupata na umeainisha gharama hiyo itumike kwa maeneo ya vijijini.

“Ni marufuku hiyo lugha ya kwamba waraka haujafika, au kwamba hiyo ni siasa, au kwamba hii ni ndani ya mita 30 au 40,” alisisitiza.

Alisema, suala la msingi wanalopaswa kufanya mameneja hao ni kuwaelewesha wananchi kwamba maombi yao yamepokelewa na wanapanga mikakati ya kuwafikishia huduma ya umeme maana ni wajibu wao kutumia ubunifu na kujipanga namna ya kuwafikia wateja, hususan wenye mahitaji ya nguzo nyingi.

Aliwahakikishia watanzania kuwa agizo la kulipia shilingi 27,000 tu kuunganishiwa umeme vijijini linatekelezeka na kwamba wale wanaohitaji nguzo nyingi wanapangiwa mpango wa kufikiwa, bali wote watahudumiwa kwa bei hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrence Maro, alisema ofisi yake imepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na kuahidi kuwa watayatekeleza kikamilifu.

“Tangu agizo la kuwaunganisha wateja wa vijijini kwa shilingi 27,000 litolewe, tumeshaunganisha wananchi 3,195 katika kipindi cha mwezi Mei, Juni na Julai mwaka huu. Tunaendelea na zoezi hilo, hivyo wananchi wenye uhitaji njooni mtuone na tutawahudumia,” alisema.

Katika ziara hiyo ya siku mbili, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji kadhaa pamoja na kuzungumza na wananchi wa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme ambapo aliwaeleza mikakati iliyopangwa na serikali kuwafikishia huduma hiyo.

118 thoughts on “Serikali Yazigeukia Kampuni Zinazotandaza Nyaya z Umeme Kwenye Majengo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama