Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Kupitia Upya Mkataba wa Ujenzi Kituo cha Forodha Horohoro- Tanga

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakikagua Scana katika Kituo cha pamoja cha Forodha katika eneo la Horohoro Mkoani Tanga ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa kukosa umeme jambo lilololeta shaka kwa usalama bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Damas Ndumbaro (kulia), wakihoji namna ambavyo Kituo cha pamoja cha Forodha – Horohoro kinavyotunza kumbukumbu za vyombo vya moto vinavyoingia na kutoka, kwa kuwa hawakulidhika na idadi ya magari ambayo yalipita kwa siku mbili, jambo lililotia shaka ukusanyaji wa mapato Kituoni hapo. Katikati ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji Kituo cha pamoja cha Forodha – Horohoro Bw. Antony Kasitu.

Na Peter Haule, WFM, Tanga

Serikali imetoa agizo kwa watendaji wa Kituo cha pamoja cha Forodha Mpakani- Horohoro, kuwasilisha nyaraka za ujenzi wa Kituo hicho ukiwemo mkataba kwa kuwa miundombinu iliyopo haijakidhi viwango jambo lililosababisha kutofunguliwa rasmi kwa kituo hicho tangu mwaka 2015.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro walipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Kituo hicho ambapo hawakuridhishwa na miundombinu yake.

Dkt. Kijaji, alisema kuwa Kituo hicho hakina mawasiliano kati ya upande wa Tanzania na Kenya hivyo kutokidhi vigezo vya kuwa Kituo cha pamoja cha Forodha kati ya nchi hizo mbili.

Alisema kuwa ukosefu wa mawasiliano unasababisha urasimu katika kuwahudumia wananchi jambo linalosababisha wateja katika mpaka huo kutafuta njia nyingine ambazo sio rasmi katika usafirishaji bidhaa jambo ambalo linaathari kubwa katika ukusanyaji wa mapato.

Miongoni mwa kasoro zilizobainika wazi ni kamera maalum za usalama zinazotakiwa kufanyakazi ni zaidi ya 14 lakini zinazofanyakazi mpaka sasa ni 4 pekee jambo linalotiashaka kuhusu usalama wa Kituo hicho

Dkt. Kijaji, alisema pia, utaratibu wa wakazi wa Horohoro kwenda kupata huduma za TRA katika Wilayani Muheza usitishwe na badala yake watumishi wa Mamlaka hiyo waende kuwahudumia wananchi katika Wilaya ya Mkinga ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara wanapotaka kulipa kodi au kutafuta huduma za masuala ya forodha.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, wakikagua nmyaraka mbalimbali na kutoa agizo la kuboresha kumbukumbu ili kulisaidia Taifa katika suala la ukusanyaji wa mapato na usalama.

Aidha, Manaibu Waziri hao wameiagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Tanga kuhakikisha Jenereta la Kituo hicho cha Pamoja cha Forodha linafanyakazi ndani ya saa 24 ili kukabiliana na upotevu wa mapato katika eneo hilo kinyume na hapo hatua zingine zitachukuliwa.

Manaibu Waziri hao wametoa maagizo hayo baada ya kuelezwa kuwa jenereta halifanyikazi baada ya kuharibika kwa takribani siku 14 na kusababisha Seikali ikose mapato na kuleta usumbufu kwa watumiaji wa Kituo hicho kwani hulazimika kukaa muda mrefu kusubiri umeme urejee baada ya kukatika.

“Kutofanya kazi kwa Jenereta katika Kituo cha Forodha- Horohoro kumechangia kukosekana kwa kumbukumbu sahihi ya magari yanayopitisha bidhaa katika mpaka huo hivyo kuwa na athari katika takwimu za mapato ya eneo hilo lakini pia usalama wa Taifa”. Alisema Dkt. Kijaji

Viongozi hao wameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kutengeneza skana ya kuchunguza usalama wa mizigo na wateja wanaoingia kwenye Kituo hicho ambayo imeharibika muda mrefu hali inayohatarisha usalama wan chi, raia na mali zao

Kwa upande wake Mhe. Dkt. Ndumbaro, ameagiza kuchimbwa kwa kisima cha maji eneo hilo kwa kuwa kiasi cha Sh. milioni sita kinachotumika kuagiza maji kila mwezi kinaweza kutumika kujenga kisima cha kudumu na kuokoa fedha nyingi zisipotee.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Damas Ndumbaro wapo katika ziara mkoani Tanga na maeneo mengine katika kutatua changamoto za ukusanyaji wa mapato na suala la usalama katika mpaka wa Tanzania na Kenya.

82 thoughts on “Serikali Kupitia Upya Mkataba wa Ujenzi Kituo cha Forodha Horohoro- Tanga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama