Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli: Tuyatumie Majeshi Katika Kazi za Dharura Kuharakisha Maendeleo Kwa Wananachi

Na Mwandishi Wetu

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Viongozi na Watendaji wa Wizara, Taasisi, Wakala na Mashirika ya Umma kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)katika  kazi za dharura zinazohitaji kasi ya haraka ya utekelezaji ili kuwaletea Maendeleo Watanzania.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mahindi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale Mkoani Ruvuma leo Jumatatu (April 8, 2019), Rais Magufuli alisema JTWZ na JKT ni miongoni mwa majeshi ya vyombo vya ulinzi na usalama yanayofanya kazi zake kwa kasi kubwa katika miradi mbalimbali pindi wanapopewa dhamana na Serikali.

Aliongeza kuwa pamoja na majukumu yake ya msingi katika kusimamia masuala ya ulinzi na usalama, vyombo vya ulinzi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JTWZ) wakati wa hali ya usalama majeshi hayo yamekuwa yakitumika katika kutekeleza kazi za dharura pindi zinapotokea.

“Nawagiza Watendaji na Viongozi wa Wizara, Taasisi za Umma ndani ya Serikali kuvitumia vyema vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ikiwemo majeshi yetu ya JWTZ na JKT katika kutekeleza kazi za dharura zinatokea mara kwa mara, kwa mfano nimwemwagiza CDF sasa aunde magari ya zimamoto na kuyapeleka katika viwanja vyetu vya ndege ambapo ni miaka miwili sasa pamoja na zabuni yake kutangazwa na pesa kuwepo hakuna gari hiyo pale TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege)” alisema Rais Magufuli.

Akitolea mfano Rais Magufuli alisema kutokana na imani kubwa ya utendaji kazi wa JWTZ na JKT, Serikali imekuwa ikitoa zabuni za miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba na Ofisi za Serikali katika Miji ya Dar es Salaam, Dodoma na maeneo mengine ya nchi ambapo majeshi hayo yameweza kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu.

Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuyawezesha majeshi yote ya vikosi vya ulinzi na usalama nchini ili yaweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, ambapo alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na JWTZ katika kuunga mkono sera ya Serikali ya ujenzi wa viwanda kwa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha maji na kiwanda cha kuchakata mahindi.

Aidha Rais Magufuli alisema kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama katika miradi ya dharura kutasaidia kuharakisha maendeleo kwa Watanzania, kwa kuwa historia inaonyesha kuwa majeshi ya Tanzania ikiwemo JWTZ hayajawahi kushindwa kazi yoyote inayopewa na Serikali huku na mfano ujenzi wa ukuta katika machimbo ya madini ya Tanzanite eneo la Mererani, ambalo lilijengwa kawa kipindi cha miezi 3 tu pamoja na ukubwa na ugumu wa kazi hiyo katika eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu Kiwanda cha kuchakata mahindi cha Kambi ya JKT Mlale, Rais Magufuli  alisema Kiwanda hicho kilichojengwa kwa gharama ya Tsh Milioni 414.77 na kuwa na uwezo wa kusindika tani  400 za mahindi, hakina budi kuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma ambao sehemu kubwa wanajishughulisha na uzalishaji wa mahindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi alisema mbali na majukumu ya ulinzi wa mipaka ya nchi na ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro, Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini ikiwemo JWTZ yamekuwa yakishiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali  ikiwemo kuunga mkono sera ya Serikali ya Uchumi wa Viwanda.

Alisema kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa inapunguza utegemezi wa bajeti kwa kuhakikisha kuwa inashiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kujihusisha na shughuli za kilimo na uvuvi ili kuwezesha majeshi hayo kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.

Aliongeza kuwa katika mwaka 2019, Serikali imechukua jumla ya vijana 32,000 ikiwemo vijana 20,000 wa mafunzo kwa mujibu wa sheria na vijana 12,000 wa mafunzo ya kujitolea ambao wamekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na uzalishaji mali.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo alisema JWTZ inaendelea kuunga mkono sera ya Serikali ya kufikia uchumi wa viwanda ambapo mbali na kuzindua viwanda vya maji na mahindi, Jeshi hilo limejipanga kuongeza wigo wa uanzisha wa viwanda vingine vingi zaidi  ikiwemo viwanda vya kuchakata alizeti.

Alisema hadi sasa Jeshi hilo limeweza kupiga hatua kubwa zaidi katika uzalishaji wa malighafi mbalimbali za viwandani,  na kuweza kutengeneza sera za jeshi hilo na hivyo kusaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika hapo awali.

82 thoughts on “Rais Magufuli: Tuyatumie Majeshi Katika Kazi za Dharura Kuharakisha Maendeleo Kwa Wananachi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama