Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Mei, 2018 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa na kuwahakikishia wananchi wa Wilaya hiyo kuwa Serikali itahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika haraka na kupeleka madaktari na wauguzi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.

Majengo ambayo yameanza kujengwa ni jengo la matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mionzi (Radiology), jengo la huduma ya mama na mtoto (RCH), jengo la maabara na jengo la wodi za kulaza wagonjwa, ambapo tayari Serikali imetoa Shilingi Bilioni 4.2 na hospitali inatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Agosti 2018.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa ujenzi wa hospitali kama hiyo unaendelea katika wilaya nyingine za Mvomero, Buchosa na Siha.

Mhe. Jafo amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya na amefafanua kuwa tangu Tanzania ipate uhuru ilifanikiwa kujenga hospitali 77, lakini kwa miaka miwili na nusu Serikali ya Awamu ya Tano imetenga Shilingi Bilioni 105 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hosptali mpya 67, na pia imechukua hatua madhubuti za kuviimarisha vituo vya afya kwa kuviwezesha vituo vipya 208 kutoa huduma za upasuaji ikilinganishwa na vituo vya afya 115 vilivyokuwa na uwezo huo tangu uhuru.

Akizungumza na wananchi wa Kilolo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kilolo kwa juhudi zao katika uzalishaji mali na amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zote ziliwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ikiwemo utoaji wa elimu bila malipo ambapo inatoa Shilingi Bilioni 23.8 kila mwezi, kusambaza umeme kwa vijiji vyote Tanzania ifikapo mwaka 2021, kuongeza dawa hospitali ambapo imetenga Shilingi Bilioni 269 katika bajeti hii na kupeleka maji katika maeneo yenye uhaba wa maji.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaahidi wananchi wa Kilolo kuwa sehemu ya barabara ya Iringa – Kilolo yenye kilometa 28 ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami, itaanza kujengwa hatua kwa hatua na amewataka kuongeza juhudi katika kilimo ili waweze kunufaika na barabara hiyo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili kujihakikishia upatikanaji wa matibabu kwa kuwa Serikali inaboresha huduma za afya, na pia ameagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaanzisha mifuko ya dawa (Drug Revolving Fund) ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza halmashauri zote zilizoshindwa kutumia fedha za miradi iliyopangwa katika halmashauri hizo, zirejeshwe hazina na zipangiwe kazi nyingine.

Akiwa njiani kuelekea Kilolo Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa kijiji cha Kilambo kilichopo Iringa Vijijini ambapo amechangia Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya zahanati na shule, na amesalimiana na wananchi wa Kijiji cha Ndiwili ambako amechangia Shilingi Milioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule na zahanati.

Halikadhalika Mhe. Rais amesalimiana na wananchi wa Ipogolo katika Manispaa ya Iringa ambapo amewatahadharisha waliojenga majengo katika hifadhi ya barabara.

Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Iringa

02 Mei, 2018

 

64 thoughts on “Rais Magufuli Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama