Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

Rais Magufuli Atuma Salamu za Rambirambi Vifo vya Watu 19 Songwe, Atoa Mkono wa Pole kwa Familia ya Dkt. Kigwangalla

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali ya barabarani iliyotokea katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19.

Ajali hiyo imetokea jana tarehe 21 Februari, 2019 majira ya saa 3:15 usiku katika mteremko wa mlima Senjele ambapo lori (Semi-trailer) lililokuwa likisafiri kutoka Tunduma kwenda Mbeya Mjini lililigonga basi la abiria kwa nyuma, kisha basi hilo likaminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine (Semi-trailer) lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wote 19 waliokuwemo ndani ya basi pamoja na dereva wa lori lililogonga basi la abiria.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.Mstaafu Nicodemas Elias Mwangela kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu wote mahali pema peponi, Amina.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani Mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amefiwa na mwanae aitwaye Zul Hamis Kigwangalla jana tarehe 21 Februari, 2019 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamefika nyumbani kwa familia hiyo Mikocheni Jijini Dar es Salaam na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiongozwa na Mama wa Marehemu Dkt. Bayoum Kigwangalla wakiwa katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Nzega Mkoani Tabora. Dkt. Hamis Kigwangalla ameshatangulia Nzega ambako mazishi yatafanyika baadaye leo.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

22 Februari, 2019

37 thoughts on “Taarifa kwa Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama